
Mbeya. Winga wa Ken Gold, Bernard Morison amesema licha ya kurejea mazoezini na wenzake lakini bado hajawa fiti kucheza mechi akiomba muda zaidi kuwa sawa, huku akilia kuikosa Ligi Kuu.
Nyota huyo raia wa Ghana alitambulishwa kikosini humo dirisha dogo akiwa huru, ambapo hajacheza mechi yoyote kati ya saba iliyochezwa na timu hiyo kufuatia majeraha ya paja yaliyokuwa yanamsumbua.
Kutokana na hali hiyo, benchi la ufundi lilimpa program maalumu ya kujifua kivyake ambapo kwa sasa tayari ameungana na wenzake kujiwinda pamoja kwa ajili ya mwendelezo wa Ligi inayotarajia kuendelea Aprili 3.
Nyota huyo akiwa Yanga msimu wa 2019/20 alicheza mechi 13 akifunga mabao manne na asisti tatu, ambapo msimu uliofuata alijiunga na Simba akiifungia mabao manne na kuhusika mengine saba kati ya mechi 24.
Aidha akiwa Yanga alikumbana na mgogoro hadi kesi yake kufika Mahakama ya usuluhishi za michezo duniani (CAS) ambapo aliweza kushinda vigogo wa timu hiyo.
Ken Gold iliyopo mkiani kwa pointi 16 inatarajia kuwa uwanjani Aprili 3 kuwakaribisha Azam mchezo ambao utapigwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Morison amesema pamoja na kuanza mazoezi rasmi na wenzake lakini ataendelea kuwa nje kwakuwa hajawa fiti kuweza kucheza mechi yoyote kwa hivi karibuni ikiwamo mchezo ujao na Azam FC.
Amesema wakati akiendelea kuuguza majeraha yake, lakini anaumia sana kuona hafanyi kazi yake, huku akieleza kuwa hawezi kulazimisha kwani inaweza kumweka pabaya badala yake anasubiri muda.
“Naumia sana kuona sifanyi kazi yangu, bado sijawa tayari na ninahitaji wiki kadhaa kuweza kucheza mechi, nikilazimisha inaweza kunipa wakati mgumu zaidi.”
“Ninachofurahishwa ni namna wachezaji wanavyojituma licha ya matokeo tuliyonayo ni aibu sana mchezaji kushusha timu daraja na ndio maana mzunguko wa pili tumekuwa na mabadiliko kwakuwa tumevuna pointi 10.” amesema na kuongeza
“Matarajio yetu ni kuona kila mechi kati ya zilizosalia tunapata ushindi na kubaki salama Ligi Kuu, tunajua ugumu uliopo ila kwa muda tuliopumzika tunaendelea kujipanga vizuri,” amesema staa huyo asiyeishiwa vituko ndani na nje ya uwanja.
Kwa upande wake kocha mkuu wa timu hiyo, Omary Kapilima amesema wamekuwa na muda mzuri wa maandalizi akieleza kuwa hesabu zao ni kushinda kila mechi na wanaanza dhidi ya Azam.
“Vijana wapo fiti na kila mmoja ana matumaini na morali kubwa katika kupambania pointi tatu, tuwatoe hofu mashabiki kwamba Ken Gold itabaki salama Ligi Kuu” amesema Kapilima.
Afisa Habari wa timu hiyo, Jose Mkoko amesema kutokana na morali iliyopo na umuhimu wa mechi saba zilizobaki, uongozi umeamua kuongeza bonasi kwa wachezaji kuwatia hamasa kushinda kila mchezo.
“Tunao wadau ambao wamekuwa karibu na timu haswa tangu mzunguko wa pili ndio maana matokeo yanatia matumaini, uongozi umeongeza dau katika bonasi ya awali ili wachezaji wafanye kazi,” amesema Mkoko