Mokono ailaza KMC, Matano akipata ushindi wa pili

Mshambuliaji wa Fountain Gate, Elie Mokono ameibuka shujaa kutokana na mabao yake mawili kutosha kuwapa pointi tatu wakiichapa KMC 1-2.

Mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa leo Alhamisi Machi 6, 2025 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, ulitawaliwa na mashambulizi ya kushtukiza huku kila upande ukikataa unyonge na kucheza soka la wazi.

Wenyeji KMC walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia mkwaju wa penalti uliowekwa kimiani katika dakika ya 45+4 na mshambuliaji wao kinara Oscar Paul ambaye sasa amefikisha mabao matano.

Mkwaju huo ulitokana na kipa wa Fountain Gate, Fadhili Kisunga kumfanyia faulo Daruesh Saliboko katika eneo la hatari. Mapumziko timu hizo zilikwenda KMC ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili kocha wa Fountain Gate, Robert Matano, aliingia na mkakati wa kusaka pointi na kulipa kisasi cha timu hiyo kupoteza mchezo wa duru la kwanza ilipofungwa nyumbani na KMC 3-1.

Dakika ya 77, Mokono aliisawazishia Fountain Gate akitumia vizuri pasi ya kichwa kutoka kwa Hashim Omary ambaye aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mudrik Abdi.

Katika dakika ya 90+3, Mokono alifunga bao la pili ambalo liliihakikishia ushindi Fountain Gate huku Mokono akifikisha mabao matano. Huo ni ushindi wa pili kwa kocha Matano katika mechi saba za ligi tangu akabidhiwe kikosi hicho Januari 10, 2025.

Kwa upande wa Kocha wa KMC, Kally Ongala, kipigo hicho ni cha sita kwake kwenye ligi kati ya mechi 12 tangu Novemba 14, 2024, alipokabidhiwa mikoba ya kuifundisha timu hiyo akishinda mbili na sare nne.

Matokeo hayo yameifanya Fountain Gate kufikisha pointi 28 na kupanda hadi nafasi ya sita kutoka ya nane, wakati KMC ikisalia nafasi ya 11 na pointi 24.