
Dar es Salaam. Katika maendeleo makubwa kwa sekta ya afya nchini, Tanzania imepiga hatua kwa kuanzisha matibabu ya ubongo kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya roboti, katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI).
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Mpoki Ulisubisya ametangaza taasisi hiyo itaanza kufanya upasuaji huu wa hali ya juu wiki hii kwa kutumia teknolojia ya ‘brain neuronavigation’, inayoboresha usahihi na ufanisi katika matibabu ya magonjwa ya nyurolojia.
Akizungumza katika mkutano wa 11 wa kimataifa wa madaktari bingwa wa upasuaji wa nyurolojia na wauguzi maalumu uliofanyika jijini Dar es Salaam Jumanne, Machi 25, 2025, Dk Ulisubisya alieleza hatua hiyo imewezekana kutokana na upatikanaji wa kifaa cha kisasa cha Brain Lab Neuro-navigation system, ambacho kimetolewa kama msaada na Chuo Kikuu cha Weill Cornell kilichopo New York, Marekani.
Alisema mfumo huu unatoa mwongozo wa papo kwa hapo wakati wa upasuaji wa ubongo, hivyo kuongeza kwa kiasi kikubwa usahihi na matokeo chanya kwa wagonjwa.
“Hii inaashiria hatua muhimu katika matibabu ya magonjwa ya ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu katika MOI.
Dira yetu ya kuifanya Moi kuwa kituo bora cha upasuaji wa nyurolojia sasa inatimia. Chuo Kikuu cha Weill Cornell kimekuwa mshirika wa thamani kwa zaidi ya miaka 16, kikiendelea kusaidia maendeleo ya wataalamu wetu,” alisema Dk Ulisubisya.
Kwa sasa, MOI inashughulikia asilimia 95 ya wagonjwa wenye matatizo ya ubongo, uti wa mgongo, na mishipa ya fahamu nchini Tanzania.
Teknolojia hii mpya inatarajiwa kupunguza idadi ya wagonjwa wanaohitaji rufaa kwenda nje ya nchi, kwa kushughulikia asilimia tano iliyosalia ya wagonjwa waliokuwa wakilazimika kutafuta matibabu maalumu nje ya nchi.
Dk Ulisubisya alitoa shukrani kwa Chuo Kikuu cha Weill Cornell na Profesa Roger Hartl kwa mchango wao wa kuboresha sekta ya afya nchini Tanzania.
“Tunaishukuru sana timu ya Profesa Hartl. Kwa niaba ya MOI, Wizara ya Afya, na Serikali, tunawashukuru kwa ushirikiano wao endelevu na dhamira yao ya kuboresha huduma za afya nchini Tanzania,” aliongeza.
Akizungumza baada ya kutambuliwa kwa mchango wake na MOI, Profesa Hartl alieleza kufurahishwa na heshima hiyo.
Alisisitiza Weill Cornell itaendelea kushirikiana na MOI, hususan kwa kujenga uwezo wa ndani kupitia programu za mafunzo kwa madaktari, wauguzi, na wataalamu wa afya wa Tanzania.
“Dhamira ya MOI katika kuendeleza utaalamu wa upasuaji wa nyurolojia na kutoa matibabu ya kisasa ni ya kipekee. Tutaendelea kuunga mkono jitihada hizi kwa kutoa mafunzo na rasilimali muhimu ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma za afya za viwango vya kimataifa,” alisema Profesa Hartl.
Mkurugenzi wa huduma za upasuaji wa nyurolojia MOI, Dk Laurent Mchome, alieleza umuhimu wa ushirikiano huu endelevu, akibainisha madaktari wa Kitanzania wamenufaika kwa kupata mafunzo maalumu ya upasuaji wa nyurolojia nchini Marekani.
Mafunzo haya yamewapa ujuzi wa kufanya upasuaji mgumu na wa hali ya juu.
Mratibu wa mkutano huo, Dk Hamisi Shabani, alisisitiza umuhimu wa Global Neurosurgery Course, mpango wa kila mwaka unaoandaliwa kwa ushirikiano na Weill Cornell.
Mpango huu unalenga kuwapa madaktari na wauguzi mbinu mpya na bunifu katika upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu, hivyo kuhakikisha maendeleo endelevu katika uwezo wa upasuaji wa nyurolojia nchini Tanzania.