
Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa KMC, Abdihamid Moallin amejiuzulu nafasi hiyo ndani ya klabu hiyo huku ikielezwa anakaribia kujiunga na kikosi cha TS Galaxy ya Afrika Kusini ambacho kimeonyesha nia ya kumuhitaji baada ya kuondoka kwa Mjerumani, Sead Ramovic.
Mwananchi liliripoti juu ya taarifa za Wasauzi hao kumhitaji Moallin ambaye ameiongoza KMC katika michezo 11 ya Ligi Kuu Bara, akishinda minne, sare miwili na kupoteza mitano akiiacha katika nafasi ya saba kwenye msimamo ikiwa na pointi 14.
Taarifa kutoka ndani ya timu hizo zimeliambia Mwanaspoti kwamba, Moallin baada ya mazoezi ya asubuhi aliwaaga wachezaji na viongozi.
“Ni kweli ametuaga na ametutakia kila la heri kwa msimu uliobaki, sisi tulimpenda sana kwa sababu ya ushirikiano ambao alikuwa anatupatia lakini maisha ni safari ndefu, leo unaweza ukawa hapa kesho ukaenda kule,” kilisema chanzo chetu.
Moallin alipotafutwa kuzungumzia hilo alisema hawezi kuzungumza chochote kwani hata yeye anasikia tu kwa wengine.
“Siwezi kuzungumza hilo kwa sasa, naomba niache kwanza unitafute kesho.”
Kwa upande wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Mwakasungula alisema hana taarifa za jambo hilo, huku akiweka wazi viongozi bado wana imani na malengo naye ya muda mrefu.
Hatua ya Moallin kuhitajika na timu hiyo inajiri baada ya aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Afrika Kusini, Mjerumani Sead Ramovic kujiuzulu kutokana na matokeo mabaya, huku sasa kocha msaidizi, Adnan Beganovic akipewa jukumu hilo la kukisimamia.
Ramovic amejiuzulu mwenyewe baada ya kuiongoza timu hiyo katika michezo sita ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini bila ushindi ambapo kati yake ametoka sare miwili na kupoteza minne, akiiacha mkiani mwa msimamo kufuatia kukusanya pointi mbili tu.
Moallin anakuwa ni kocha wa pili msimu huu kujiuzulu mwenyewe kwenye Ligi Kuu Bara baada ya Fikiri Elias kuachana na KenGold kwa makubaliano ya pande mbili Septemba 17, mwaka huu kutokana na matokeo mabovu ambayo kikosi hicho cha jijini Mbeya kilikuwa nayo.
Fikiri aliiongoza KenGold katika michezo mitatu ya Ligi Kuu Bara na kupoteza yote, akichapwa mabao 3-1, dhidi ya Singida Black Stars Agosti 18, 2024, akachapwa tena 2-1 na Fountain Gate Septemba 11, 2024, kisha kupoteza kwa bao 1-0, mbele ya KMC Septemba 16, 2024.