
Baada ya kuvunja mkataba na supastaa wake Neymar Jr, timu ya Al-Hilal inataka kumsajili winga wa Liverpool na Misri, Mohamed Salah, 32, katika dirisha hili la usajili ili kuziba pengo lake.
Salah ni mmoja kati ya wachezaji wa Liverpool ambao mikataba yao inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu na hadi sasa hakuna ishara ya makubaliano juu ya kuurefusha kwa ajili ya kuendelea kukitumikia kikosi hicho.
Inaelezwa kwamba Neymar alipewa chaguo la ama kuondoka katika timu hiyo kwa mkopo au mkataba wake uvunjwe kabisa aondoke akiwa mchezaji huru.
Kwa sasa Al-Hilal wapo tayari kumpa Salah mshahara sawa au zaidi ya ule ambao Neymar alikuwa akiupata kwa wiki ambao ni takriban Pauni 2.5 milioni.
Itakumbukwa kwamba maisha ya Neymar katika kikosi cha Al-Hilal yaliandamwa na majeraha ya mara kwa mara jambo ambalo lililosababisha muda mwingi kuwa nje ya uwanja akijiuguza kwa maumivu.
ROMA inahitaji kuipata saini ya kiungo wa Manchester United na Brazil, Casemiro, 32, kwa mkopo wa nusu msimu, lakini dili hilo litakamilika ikiwa tu itafanikisha mpango wa kumuuza staa raia wa Argentina, Leandro Paredes, 30. Mkataba wa sasa wa Casemiro huko Manchester United unatarajiwa kumalizika mwakani. Msimu huu amecheza mechi 22 za michuano yote.
NAPOLI na Juventus zinamfuatilia kwa karibu straika wa Manchester United na Denmark, Rasmus Hojlund, 21, na kuna uwezekano mkubwa zikatuma ofa kwa ajili ya kumsajili katika dirisha hili la majira ya baridi au kiangazi. Mchezaji huyo hajaonyesha kiwango bora chini ya kocha Ruben Amorim, jambo linalosababisha timu nyingi kutaka kuipata huduma yake hata kwa mkopo.
MANCHESTER United ipo katika hatua za mwisho kukamilisha uhamisho wa kumsajili beki wa pembeni wa Lecce na Denmark, Patrick Dorgu, 20, katika dirisha hili kwa ada ya uhamisho inayokadiriwa kufikia Pauni 30 milioni. Inaelezwa Dorgu ameridhia kujiunga na Man United, lakini changamoto kubwa iliyochelewesha dili hili ilikuwa ni ada ya uhamisho.
MABOSI wa Wolves wanatarajia kupokea ofa kutoka timu nyingine mpya juu ya mshambuliaji raia wa Brazil, Matheus Cunha, 25, kabla ya dirisha hili kufungwa. Wolves inataka kupokea ofa nyingi zaidi kabla ya kuamua wapi inaweza kumuuza staa huyo. Hadi sasa Aston Villa, Arsenal na Nottingham Forest zimeshawasilisha ofa kwa ajili ya kumsajili.
DILI la kiungo wa Juventus, Douglas Luiz kujiunga na Manchester City kwa mkopo katika dirisha hili linazidi kufifia kutokana na kutofikia mwafaka baina ya timu hizo. Mabosi wa Juventus wanataka kuwepo kipengele kitakachowalazimisha Man City kumnunua jumla baada ya muda wake wa mkopo kumalizika. Luiz mwenye umri wa miaka 26, mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2029
STRAIKA wa Bayer Leverkusen na Nigeria, Victor Boniface, 24, amepewa ruhusa ya kutohudhuria mazoezi juzi na jana kwa kile kinachotajwa kwamba anajiandaa kutimkia Saudi Arabia kujiunga na Al-Nassr. Boniface ambaye msimu huu amecheza mechi 15 za michuano yote na kufunga mabao manane mkataba wake na Leverkusen unamalizika 2028.
CHELSEA imekubali ofa ya Euro 12 milioni kutoka Lazio inayohitaji saini ya kiungo raia wa Italia, Cesare Casadei, 22, ambaye hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha Chelsea. Katika mkataba wa mauziano, Chelsea imeweka kipengele cha kulipwa asilimia 25 ya ada ya uhamisho ikiwa atauzwa kwenda timu nyingine.