
SIKU moja baada ya kiungo wa Simba, Charles Ahoua kukosa nafasi ya wazi ambayo ingeisaidia timu hiyo kushinda mabao mawili dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini kwenye uwanja wa nyumbani, mwekezaji wa timu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ amemkingia kifua.
Simba ilicheza na Stellenbosch jana katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo ilishinda bao 1-0.
Katika mchezo huo Ahoua ndiye alikuwa mfungaji wa bao pekee kwenye mechi hiyo ya mkondo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika iliyochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar, jana.
Kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii Instagram, Dewji ameandika, “Charles Ahoua ni mmoja wa wachezaji waliotupa sababu nyingi za kushangilia msimu huu, licha ya vyote amekuwa sehemu ya mafanikio yetu;
“Kwa kosa moja lililtokea tunaweza kumsema vibaya leo, ila tukumbuke hata mastaa wa dunia kama Fernando Torres waliwahi kukosa magoli ya wazi kwenye mechi kubwa kama Chelsea dhidi ya Manchester United. Hii ni soka. Haya ni mambo ya kawaida kwenye mchezo huu.”
Pia alitumia nafasi hiyo kuwataka mashabiki wa Simba kusimama na kiungo huyo baada ya tukio lililotokea akisema: “Tunajifunza, tunaimarika na tunaendelea kupambana.”
Ameandika kuwa mchezo wao dhidi ya Stellenbosch bado uko mbele na kwamba safari haijaisha.
“Na huu si wakati wa kulaumiana, ni wakati wa kuungana na kuwa kitu kimoja.
Simba inajengwa juu ya mshikamano. Tunasimama na Ahoua. Tunasimama na kila mchezaji anayejitoa kwa jezi hii na tunaendelea na vita iliyokua mbele yetu.”
Simba itashuka uwanjani jijini Durban, Afrika Kusini Jumapili wiki hii kwa ajili ya mchezo wa pili dhidi ya wapinzani wao ambao utaamua timu itakayotinga fainali ya mashindano hayo.