Mnyika ataka utamaduni wa Chadema ulindwe

Shinyanga. Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendelea (Chadema), John Mnyika amewataka wananchi wa Shinyanga kulinda haki na utamaduni wa Chadema wa kutetea haki badala ya kukimbilia ubunge.

Mnyika ametoa kauli hiyo wakati kukiwa na vuguvugu la wanachama wa Chadema wanaojivua uachama wao kwa madai ya kutokubaliana na kaulimbiu ya chama hicho ya No reforms, No election (Bila mabadiliko, hakuna uchaguzi) huku wakilenga kuzuia uchaguzi.

Makada hao wameeleza dhamira yao ya kutaka kugombea ubunge, huku wakieleza kwamba Chadema kutosimamisha wagombea kwenye uchaguzi ujao, chama hicho kitakwenda kufa kwani haiwezekani kuzuia uchaguzi.

Akizungumza leo Mei 16, 2025 katika mkutano na wananchi uliofanyika katika Uwanja wa Jasko uliopo katika Kata ya Ngokolo, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, amesema anahitaji haki itendeke.

“Wanaosema tunawachelewesha kupata haki zao za kugombea ubunge, chama chetu hakiko kwa ajili ya ubunge au uongozi wowote, bali kipo kwa ajili ya haki, ni bora tuchelewe lakini tulinde utamaduni wa chama,” amesema Mnyika.

Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema Taifa, Godbless Lema amesema hawajasusia uchaguzi bali wanataka haki na watawashawishi wananchi kuzuia uchaguzi kwa njia ya amani.

“Hatutaki kupendelewa tunataka haki itendeke tunawashawishi wananchi wananchi wazuie uchaguzi kwa njia ya amani wala si machafuko siku zote tunataka amani,” amesema Lema.

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti, Lucas Ngoto amesema kuwa hawaogopi uchaguzi lakini wanataka kusimamia kile kilicho haki kwa Watanzania.

“Sisi hatuogopi uchaguzi hata kama uchaguzi ukichukua miaka miwili kufanyika au kesho asubuhi ukifanyika tuko tayari ila tu kuwe na tume huru,” amesema Ngoto.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *