Mnamzingatia lakini Nasoro Saadun?

Miongoni mwa wachezaji walioibuka kama sapraizi msimu huu wa Ligi Kuu Bara ni Nassor Saadun Hamoud, kiungo mshambuliaji wa Azam FC aliyesajiliwa kutoka Geita Gold.Wengi hawakumpigia hesabu kwamba angekuwa mmoja wa wachezaji muhimu kwa matajiri hao wa Chamazi, hasa kutokana na majina makubwa mengine yaliyosajiliwa na klabu hiyo.

Hata hivyo, Saadun ameonyesha kiwango cha juu, akicheza kwa ujasiri na bila presha kubwa, kitu ambacho kinamfanya kuwa msaada katika kikosi hicho.

Kocha wa Azam FC, Rachid Taoussi, hakusita kumzungumzia mchezaji huyo. “Nassor  ni kijana mwenye nguvu na anajua anachokifanya uwanjani. Ana kasi na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira. Yeye ni mchezaji ambaye anaweza kuleta mabadiliko katika timu wakati wowote,” anasema kocha huyo akionekana kutambua nafasi muhimu ya Saadun katika kikosi chake.

KUANZA TARATIBU

Saadun alianza taratibu kupata nafasi ya kucheza akiwa chini ya kocha Youssouph Dabo, ambaye baadaye alifutwa kazi kutokana na kuanza vibaya msimu huu. Akiwa Morocco, alifunga bao katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Union de Touarga, ambapo walitoka sare ya 1-1. Uwezo aliouonyesha kwenye mchezo huo ulikuwa ni dalili ya kipaji chake na jinsi alivyokuwa na uwezo wa kutumia nafasi chache alizopata kuonyesha kuwa anaweza kuwa msaada mkubwa kwa kikosi cha Azam FC.

Alipopewa nafasi zaidi chini ya kocha mpya, Rachid Taoussi, Saadun hakusita kuthibitisha thamani yake. Aliweza kufunga bao la kuvutia katika mchezo dhidi ya KMC. Goli hilo liliwaacha mashabiki wa soka na midomo wazi kwa namna alivyowazunguka mabeki wa KMC na kumzidi ujanja kipa wao, Fabien Mutombora, wakati Azam FC ikipata ushindi wa mabao 4-0. Bao hilo lilikuwa ishara ya kipaji cha Saadun na uwezo wake wa kucheza mbele ya mabeki wenye uzoefu.

MOTO ULIVYOWAKA 

Mchezo dhidi ya KMC ulikuwa tu mwanzo wa moto aliouanza. Katika mchezo uliofuata dhidi ya Coastal Union, Saadun alirudia kile kile ambacho mashabiki wengi walikuwa wameanza kumzoea: uwezo wa kufunga mabao ya aina ya kipekee. Akiunganisha kasi yake na ufundi, alifunga bao lingine lililofanana na yale ambayo Lionel Messi amekuwa akifunga kwa miaka mingi. Kutokana na kiwango chake bora kwenye mchezo huo, Saadun alipewa tuzo ya mchezaji bora wa mechi, jambo lililoimarisha imani ya benchi la ufundi na mashabiki kwake. 

Akizungumzia kiwango chake, Saadun alisema, “Najisikia vizuri kwa jinsi kiwango changu kinavyokubalika. Ninapenda kujituma na kufanya kazi kwa bidii ili niweze kusaidia timu yangu. Tuzo ya mchezaji bora wa mechi ni motisha zaidi ya kuendelea kujituma na kufikia malengo yangu binafsi na ya timu.”

Kiwango cha Saadun hakikuwa bahati nasibu. Baada ya mchezo dhidi ya Coastal Union, Saadun aliendelea kung’ara. Kiwango bora alichoonyesha kilimfanya uongozi wa Azam FC kumuongeza mkataba mpya wa miaka miwili, baada ya awali kupewa mkataba wa mwaka mmoja tu wakati walipomsajili kutoka Geita Gold. Mkataba huu mpya ni ishara ya imani kubwa waliyonayo kwa mchezaji huyu kijana, ambaye ameanza kuwa nguzo muhimu kwenye safu ya ushambuliaji ya Azam FC.

KUTAMBULIKA KIMATAIFA 

Kutokana na kiwango chake bora, Saadun alipata nafasi ya kuitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Hemed Suleiman ‘Morocco’, kwa ajili ya michezo ya kufuzu kwa fainali za mataifa ya Afrika (AFCON) dhidi ya DR Congo.

Saadun alipata nafasi ya kucheza katika mchezo wa kwanza uliofanyika Kinshasa, ingawa Taifa Stars walipoteza kwa bao 1-0. Hata hivyo, wito wake katika timu ya taifa ni ishara ya kuthaminiwa kwa uwezo wake, na pia ni hatua muhimu kwake katika kuendeleza kipaji chake na kukua zaidi kwenye soka la kimataifa.

Baada ya wiki hiyo ya kimataifa, Saadun aliendelea kuonyesha moto wake kwenye Ligi Kuu. Alifunga bao lake la tatu msimu huu katika ushindi wa mabao 2-0 wa Azam FC dhidi ya Tanzania Prisons, mchezo uliochezwa ugenini. Bao hili lilionyesha kwamba Saadun si mchezaji wa kubahatisha bali ana uwezo wa kweli wa kuchangia mafanikio ya timu yake katika kila mchezo.

HISTORIA YAKE

Saadun alizaliwa Temeke, Dar es Salaam, Machi 23, 2001. Safari yake ya soka ilianzia kwenye kikosi cha vijana cha Mtibwa Sugar msimu wa 2017/18, ambacho kilikuwa na wachezaji wengine nyota kama Onesmo Mayaya na Dickson Job.

Akiwa Mtibwa, Saadun alicheza kama winga, lakini mara kwa mara alicheza kama mshambuliaji wa kati akipishana na Abdul Haule na Onesmo Mayaya.

Baada ya kujizolea uzoefu wa soka la vijana, Saadun alipata fursa ya kucheza nje ya nchi. Alianza safari yake ya kimataifa katika klabu ya Tersana ya Misri, kabla ya kutimkia Serbia kucheza Ligi ya Belgrade Zone. Akiwa huko, aliwahi kuichezea timu za Žarkovo na Šumadija Aranđelovac, kabla ya kurejea nchini.

Kipindi alichokuwa nje kilimfundisha mengi kuhusu soka la kasi na ushindani, jambo ambalo limekuwa faida kubwa kwake akirejea kucheza kwenye Ligi Kuu ya Tanzania.

TUMZINGATIE

Saadun ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa, kasi ya ajabu, nguvu, na uwezo wa kutumia nafasi alizozipata. Hadi sasa, amefunga mabao matatu kwenye Ligi, lakini kocha Rachid Taoussi anaamini kuwa Saadun ataendelea kung’ara zaidi.

“Nina imani kubwa na Nassor . Kama ataendelea kupata muda wa kucheza, naamini atafunga mabao zaidi ya kumi msimu huu,” anasema kocha huyo.

Kwa Saadun, kila mchezo ni fursa ya kuthibitisha uwezo wake, na ana kila sababu ya kuendelea kufanya vizuri. Akipata muda wa kutosha kucheza, Saadun anaweza kuwa miongoni mwa washambuliaji hatari zaidi msimu huu, na Azam FC watakuwa na silaha kali ya kushinda michezo mingi mbele yao.