Mmoja afariki, 33 wajeruhiwa ajali ya Coaster na katapila

Songwe. Mtu mmoja amefariki dunia na wengine 33 kujeruhiwa katika ajali ya basi dogo aina ya Toyota Coaster lililogongana na katapila, iliyotokea jana mchana eneo la Msinde Wilaya Momba mkoani Songwe.

Kamanda wa Polisi mkoani Songwe, Augustino Senga amesema ajali hiyo imetokea jana Machi 10, 2025 saa sita mchana ikihusisha gari aina ya Toyota Coaster na katapila.

Amesema Coaster hiyo inafanya kazi ya kusafirisha abiria kati ya Ileje na Mbeya mjini.

Kamanda Senga amesema gari hilo, linalomilikiwa na Bobu Mwampashi, lilikuwa likiendeshwa na Juma Rojala (47), ambaye alipata majeraha na anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe.

Kamanda Senga pia amesema kuwa mwanamke mmoja, aliyefahamika kwa jina la Sara Mzopola (37), alifariki dunia akiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya mji wa Tunduma, iliyopo Mpemba.

“Kwa taarifa za awali, chanzo cha ajali hiyo ni kwamba dereva wa katapila alishindwa kulidhibiti na kugongana na gari hilo, hali iliyosababisha majeraha kwa abiria na kifo cha mmoja wao,” amesema Kamanda Senga.

Amesema pia kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta dereva wa katapila aliyetoweka eneo la tukio baada ya kusababisha ajali hiyo, na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Akizungumza na Mwananchi leo Machi 11, 2025 Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Sebastiani Siwale, amethibitisha kupokea majeruhi 33 huku baadhi yao wakiwa wamevunjika miguu na mikono.

Siwale amesema kuwa kati ya majeruhi 33, 10 walikuwa na hali mbaya, kwani walikuwa wamevunjika miguu na mikono, na walielekezwa kupatiwa matibabu katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Songwe, iliyopo Vwawa.

Amesema mwanamke mmoja amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu na mwili wake umehifadhiwa hospitalini hapo.

“Majeruhi 14 kati ya  33 wamepatiwa matibabu na kuruhusiwa, kwani hali zao zilikuwa nzuri. Wengine wanane pia wataruhusiwa leo kutokana na wanavyoendelea,” amesema Siwale.