Mloganzila: Ushindi wa Profesa Janabi ishara kuimarika huduma za afya

Mloganzila: Ushindi wa Profesa Janabi ishara kuimarika huduma za afya

Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila, imetoa pongezi kwa Profesa Mohamed Janabi kufuatia ushindi wake wa kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, ikieleza hatua hiyo ni ishara ya kuimarika kwa huduma za afya nchini huku ikisisitizwa umuhimu wa kuanzishwa viwanda vingi vya dawa na vifaatiba ndani ya nchi.

Profesa Janabi alichaguliwa kushika nafasi hiyo baada ya kupata kura 32 kati ya 46, ambapo alihitaji kura 24 ili kushinda.

Akizungumza leo Mei 22, 2025 katika hafla ya kupokea msaada wa sindano zenye thamani ya Sh25 milioni kutoka kampuni ya Kitanzania ya Partners Group Limited, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Tiba MNH–Mloganzila, Dk Elineema Meda amesema ushindi wa Profesa Janabi unaonesha hadhi ya Tanzania katika sekta ya afya barani Afrika.

Akiuzungumzia msaada uliotolewa na kampuni ya Patners group Limited, Dk Meda amesema umetolewa na wazawa walioona jitihada zinazofanywa na Serikali katika utoaji huduma kwenye hospitali hiyo na kueleza umuhimu wa kuwa na viwanda vya vifaa tiba na dawa vya kutosha.

“Msaada huu wa sirinji ni muhimu, kabla hatujaupokea, ombi la vijana hawa lilipitia kwangu kama mkurugenzi wa huduma za tiba, ilibidi niwasiliane na wenzangu kwa sababu hizi sindano hazitumiki kwa kila mgonjwa zina sehemu maalumu.

“Baada ya kujiridhisha, Mkuu wa idara ya watoto akanishauri kwamba tukizipokea zitatufaa, nilitaka kupata uhakika wa afisa manunuzi pia kwamba hatuchukui kitu ambacho hakina ubora, kisha baada ya muda tukatumia pesa ya Serikali kuziharibu,” amesema na kuongeza;

“Sisi huwa hatupokei kila msaada, kuna nyakati tunakata, huu wa wenzetu hawa tulijiridhisha ni sindano zenye ubora, tutazitumia kwa weledi ili kuhakikisha tunaendelea kutoa huduma bora kwa watoto kwa sababu zinakwenda kutumika kwao.”

Akieleza changamoto za dawa na vifaa tiba, Dk Meda amesema mara nyingi inashindikana kutoa huduma nzuri kwa sababu ni ghali.

Amesema Tanzania haizalishi dawa nyingi sambamba na vifaa tiba, jambo alilosema linasababisha huduma ziwe ghali na haziko sawa  kwa sababu waaangiza kutoka nje ya nchi.

“Tukiona Watanzani wanafungua viwanda ndani huo ni mwanzo mzuri wa kuona upatikanaji wa vifaa kwa urahisi na huduma zitakuwa za bei ya chini katika ubora ule ule kama ilivyo kwa vijana wa Patners Group Limited,” amesema.

Mkurugenzi wa Patners Global Group Limited, Rashid Baraka amesema kampuni hiyo imeamua kutoa msaada huo kwa kutambua jitihada zinazofanywa na Serikali pamoja na wataalam hao katika kuwahudumia wananchi kwa moyo na unyenyekevu

“Hii ni sehemu ya kampuni katika kurudisha kwenye jamii, tumetoa vifaa hivi ambazo ni sindano 30,000 zenye thamani ya Sh25 milioni kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za Serikali katika afya,” amesema.

Aizungumzia unafuu wanaopata vifaa tiba kutengenezwa nchini, James Kalema kutoka Afya Lead amesema kunasaidia kupunguza gharama za huduma.

“Kampuni yetu inapaki vifaa vya kujifungulia kwa mama mjamzito, kabla ya kufanya kazi na Patners Group Limited, vifaa hivi vilipatikana nwa Sh18,000 na sasa tunashirikiana na Patners group Limited, tunavipaki kwa Sh12,000,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *