Mlinzi wa shule mbaroni tuhuma za kumdhalilisha kingono mwanafunzi

Mtwara. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara linamshikilia Abdalah Hassani Masangule (56) mlinzi wa Shule ya Sekondari Tandika na mkazi wa Mtaa wa Mmingano kwa tuhuma za udhalilishaji wa kingono.

Katika taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Machi 1,2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Issa Suleiman imesema mtuhumiwa amekuwa akimfanyia vitendo vya unyanyasaji mwathirika (jina limehifadhiwa) miaka 11, mwanafunzi wa darasa la tatu (jina la shule limehifadhiwa).

“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa alianza kujenga ukaribu na mtoto huyo kisha kumlaghai na kutekeleza kitendo hicho.

“Upelelezi wa shauri hilo unaendelea na utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani,”imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Katika hatua nyingine  Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara limeeleza kufanya uchunguzi wa tukio la kujipiga risasi kwa mlinzi wa Kampuni ya Kiwango Security, Shadrack Chama Kisinza (36), lililosababisha kifo chake.

Tukio hilo linaelezwa kutokea Februari 25, 2025, katika Kijiji cha Hiari ndani ya Kiwanda cha Saruji cha Dangote wakati mlinzi huyo akiwa kazini.

Hata hivyo jeshi hilo limesema halitakuwa na muhali kumchukulia hatua za kisheria mtu yeyote atakayejaribu au kufanya vitendo vya ukatili, unyanyasaji na udhalilishaji wa aina yoyote ile.

“Pia, wananchi wanasisitizwa kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu katika maeneo wanayoishi kupitia viongozi wa serikali au mamlaka zinazotambulika kisheria ili hatua za haraka zichukuliwe,”imesema taarifa hiyo.