Mlandizi, Ceasiaa mechi ya matumaini

LIGI itakaporejea kuna mechi kali tano zitakazopigwa viwanja mbalimbali ikiwemo Ceasiaa Queens itakayokuwa ugenini dhidi ya Mlandizi Queens ukiwa ni muendelezo wa raundi ya 13 Ligi Kuu Bara.

Mchezo huo ni moja kati ya mechi ya matumaini kwa pande zote mbili, Mlandizi inayotaka kujinasua mkiani, ikiweka rekodi ya kuwa timu pekee ambayo haijaonja ushindi WPL na ina pointi moja ikifungwa jumla ya mabao 64 na kufunga tano, huku Ceasiaa ikitaka kupanda nafasi kutoka ya saba hadi ya tano, ikiwa na pointi 13 hadi sasa.

Ceasiaa kwenye michezo 10 imepata ushindi mechi tatu sare moja na kupoteza sita ikifunga mabao 10 na kuruhusu 24.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha wa Ceasiaa, Ezekiel Chobanka alisema mipango ya timu hiyo ni kupata ushindi wa pointi tatu kwenye mchezo huo ambao anaamini itatoka nafasi iliyopo na kusogea juu.

“Ligi imekuwa ngumu lakini tunajitahidi kupambana nayo, mipango yetu kama itakuwa sawa tuchukue alama tatu kwa Mlandizi ili tupande na nashukuru kikosi chetu kwa sasa kimebadilika,” alisema Chobanka.

Kwa upande wa Kocha wa Mlandizi, Jamila Rajabu alisema ni mchezo mgumu wanaokwenda kukutana nao, lakini watapambana hadi mwisho kupata angalau pointi tatu nyumbani.

“Tuna changamoto kubwa hatujapata ushindi wowote kwenye ligi, inatupa ugumu, tutajitahidi tukiwa uwanja wetu wa nyumbani kupata ushindi japo sio rahisi.”