
USHINDI wa mabao 3-0 iliyopata Mlandege dhidi ya Kipanga na ule wa KVZ iliyoinyoa Mwembe Makumbi City, umeziweka timu hizo mbili katika nafasi nzuri ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) ambao umetemwa mapema na waliokuwa watetezi, maafande wa JKU.
Mlandege ilipata ushindi huo jana jioni katika mfululizo wa mechi za ligi hiyo iliyosaliwa na raundi moja ili kufunga msimu, nne zikipigwa jioni ya leo, umeifanya iendelee kuganda kileleni ikifikisha pointi 59 kama ilizonazo KVZ na bingwa mpya anatarajiwa kufahamika Ijumaa ya wiki hii.
Mabao ya Laureny Rolenzo katika dakika 30, Abdallah Idd Pina dk 51 na lile la Mussa Hassan la dk 65 yaliifanya Mlandege kujiweka pazuri kama itamaliza na ushindi mbele ya New City iliyokwisha kushuka daraja mapema kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa mbele ya maafande wa KVZ.
KVZ iliyoshinda 2-1 pia jana kwenye Uwanja wa Mao, Unguja kupitia mabao ya Michael Joseph aliyefunga yote katika dakika ya 56 na 66 kabla ya Robert Pius kuipatia bao la jiooni Mwembe Makumbi ambayo iliongoza msimamo wa ligi hiyo kwa muda mrefu kabla ya kuchemsha mwishoni.
Matokeo hayo yamezifanya timu hizo kulingana pointi na kila mmoja ikiombea mwenzake achemshe katika mechi ya mwisho ili kutangazwa bingwa wa msimu huu.
Mlandege inaongoza msimamo kwa kufunga mabao 63 na kufungwa 19, wakati KVZ ina 34 na kufungwa 12 na timu yoyote itakayozingua Ijumaa inaweza kujikuta ikiwaachia wapinzani wao kubeba taji hilo lililotemwa na JKU iliyolitwaa msimu uliopita ambayo kwa sasa ipo nafasi ya tano kwa pointi 49.
Kutokana na hofu ya kuwapo kwa upangaji wa matokeo, Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) limeamua kuzipanga mechi hizo muda mmoja kwenye Uwanja wa Mao A na Mao B vilivyopo Unguja kuanzia saa 10:00 jioni ili kutafuta bingwa, wakati mechi za kumalizia msimu kwa timu nyingine zikianza kupigwa leo na kesho. Mlandege inasaka taji la nane la ligi hiyo wakati KVZ inasaka taji la kwanza.
Kwa mujibu wa ratiba leo kuna mechi nne ambapo saa 8 mchana kwenye Uwanja wa Finya, Pemba Tekeleza iliyoshuka daraja ilikuwa mwenyeji wa Zimamoto na saa 10:00 jioni hii, Mwenge inayopambana kuepuka kushuka daraja itaumana na Inter Zanzibar iliyoshuka mapema. Kati ya Mwenge na Junguni United moja wapo itashuka daraja.
Junguni inapambana isiungane na zilizoshuka kwa kuvaana na mabingwa wa kihistoria wa ligi hiyo, KMKM kwenye Uwanja wa Mao B, wakati Mafunzo inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 55 inaumana na Chipukizi ya Pemba kwenye Uwanja wa Mao A.
Timu zilizoshuka daraja hadi sasa ni tatu ikiwamo New City, Tekeleza na Inter Zanzibar zilizopanda msimu huu sambamba na Junguni United kabla ya kushindwa kushikilia bomba na sasa imesalia timu moja ya kuungana na timu hizo ili kuzipisha timu nne zilizopanda kutoka Ligi Daraja la Kwanza kanda ya Pemba na Unguja.
Timu zilizopanda daraja kwa ajili ya msimu ujao kwa Ligi hiyo ni; Wawi Stars na Fufuni kutoka Pemba na maafande wa Polisi na New King kutokea Unguja. Polisi ilishuka daraja misimu miwili iliyopita.