
BINGWA wa mbio za magari mwaka 2024, Manveer Birdi anatarajiwa kuanza kwenye mashindano ya ufunguzi wa msimu ya Mkwawa Rally of Iringa, yanayotarajiwa kuchezwa mwezi Mei, mwaka huu, mkoani Iringa.
Birdi alidhihirisha ubora wake katika mashindano ya raundi mbili ya rally Sprint, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam kwa kuibuka bingwa na sasa anakabiliwa na mtihani katika ufunguzi wa mbio hizo anazokwenda kama bingwa mtetezi akiwa pia ni bingwa wa taifa wa msimu uliopita.
Mwenyekiti wa Klabu ya Mbio za Magari Iringa (IMSC), Robert Maneno alithibitisha jana maandalizi, zikiwemo pia barabara ambazo magari yatatumia, yameanza kwa kasi tangu juma lililopita na Birdi atakuwa na kibarua kizito kaifikia azma yake ya kutetea ubingwa.
Aliwataja madereva kama Yassin Nasser, Ahmed Huwel, Randeep Singh, Harrinder Deere na Gurpal Sandhu wanatarajiwa kumpa upinzani mkubwa bingwa huyu mtetezi.
“Tunatarajia Yassin Nasser atakuja Iringa baada ya kumalizika kwa mbio za magari za ubingwa wa Africa, Pearl of Africa Rally pamoja na mwenyeji Ahmed Huwel na Randeep Singh kama wapinzani wa Birdi katika mbio hizi.”
Alisema mashindano hayo yataanza rasmi Mei 24, katika Uwanja wa Samora, mjini Iringa na kumalizika Mei 25 katika Shamba la Mt Huwel, nje kidogo ya mji huo zikiwa ndiyo raundi ya ufunguzi wa msimu wa mbio za magari za ubingwa wa taifa mwaka huu na anatarajia kuona madereva wengi wakishiriki ili kupata pointi za kwanza za msimu.
Maneno alisema hadi mwishoni mwa juma lililopita, madereva kutoka mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Morogoro, Tanga na wenyeji Iringa ndio waliothibitisha kushiriki katika mbio hizo.
Alisema anatarajia timu ya Harri Singh Kutoka Kilimanjaro itakuwepo, wakati Samir Shanto, Waleed Nahdi, Ethan Taylor wakitajwa kama madereva wakali kutoka Morogoro.
Manveer Birdi, Randeep Singh na Harrinder Deere ni vinara wa mbio za magari kutoka Mkoa wa Dar es Salaam.