Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ameahidi kusimamia kwa ukaribu utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri ambayo ni utekelezaji wa malengo ya serikali ya kuyawezesha kiuchumi makundi mbalimbali ya kijamii yakiwemo ya wanawake, vijana, na wenye ulemavu.
Akizungumza katika Kongamano la Jukwaa la Wanawake Wajasiriamali wilaya Ilala lililofanyika leo tarehe 14 Juni 2025 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, DC Mpogolo amesema kuwa mkopo huu ni sehemu ya mikakati mikuu ya Serikali ya Awamu ya Sita ambayo inalenga kuwezesha wanawake kuwa na nguvu za kifedha na kujikwamua kiuchumi.
“Serikali ya Awamu ya Sita imetupa maelekezo thabiti kuhakikisha mikopo hii inawafikia walengwa hasa wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu. Tutaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wake kwa uwazi na usawa bila kupendelea wala kuangalia upande wowote,” amesema DC Mpogolo.
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya ameongeza kuwa jiji hilo limetenga zaidi ya Shilingi Bilioni 5 kwa ajili ya mikopo hiyo kwa wanawake likiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kuimarisha nafasi ya mwanamke katika uchumi wa taifa.
Mabelya pia amesisitiza kuwa maandalizi ya utoaji rasmi wa mikopo kwa vikundi vilivyoidhinishwa yamekamilika na mchakato wa utoaji wa mikopo hiyo utazingatia sheria, kanuni mpya na mfumo wa kibenki.
Jukwaa la Wanawake Wajasiriamali wa Ilala lililofanyika leo limewakutanisha wanawake kutoka kada mbalimbali wakiwemo waliowahi kuhudumu katika nyadhifa mbalimbali kwenye serikali kuu akiwemo aliyewahi kuwa waziri wa fedha, Zakia Meghji.
Imeandaliwa na @moseskwindi