Mkuu wa teknolojia wa Ulaya anatoa wito kwa Marekani kwa ushirikiano zaidi

Henna Virkkunen, kamishna wa sera za kidijitali wa Umoja wa Ulaya, ametoa wito siku ya Ijumaa kuwepo kwa ushirikiano wa karibu kati ya Marekani na Ulaya kuhusu udhibiti wa teknolojia, suala ambalo linagawanya Brussels na Washington.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

“Kampuni kubwa za teknolojia zinajua kuwa ushirikiano wa karibu wa udhibiti ungekuwa wa manufaa kwa biashara zao,” Virkkunen ameliambia shirika la habari la AFP baada ya kukutana na watendaji wakuu wa Silicon Valley, ikiwa ni pamoja na Mark Zuckerberg wa Meta na Tim Cook wa Apple.

Ziara ya Virkkunen huko California na Washington ilikuwa ya kwanza tangu ateuliwe kwenye wadhifa huo mwishoni mwa mwaka jana, huku Umoja wa Ulaya ukikamilisha uchunguzi kuhusu makampuni makubwa ya Marekani kwa kukiuka sheria zake.

Rais Donald Trump aliingia madarakani mwezi Januari, akichukua msimamo mkali dhidi ya sera za Ulaya ambazo anasema zinaiadhibu Marekani isivyo haki.

Mstari huu mkali umekaribishwa na baadhi ya wakuu wa teknolojia, hasa Mark Zuckerberg, ambaye anaishinikiza Ikulu ya Marekani kujibu Brussels.

Anafananisha sheria za teknolojia za Ulaya na ushuru unaopaswa kuwa mezani katika vita vya kibiashara vya Donald Trump na Ulaya.

Henna Virkkunen anabaini kwamba ushawishi wa Mark Zuckerberg kwa rais wa Marekani ulikuwa wa “kawaida” kwa makampuni makubwa yanayotaka kutetea maslahi yao.

Lakini “Sheria za Ulaya ni sawa kwa makampuni ya Ulaya, Asia na Marekani, hivyo si vikwazo vya kibiashara,” ameongeza.

Wakati wa ziara yake yanchini Marekani, Bi Virkkunen pia alikutana na maafisa wakuu wa Marekani, ambao wengi wao walielezea Udhibiti mpya wa Huduma za Kidijitali wa EU (DSA) kama aina ya udhibiti wa serikali.

DSA inahitaji makampuni kufuatilia ipasavyo maudhui ya mtandaoni, au kutozwa faini ya hadi 6% ya mauzo ya kila mwaka ya kampuni duniani kote.

Kamishna, anayehusika na utekelezaji wa DSA, amesema kuwa mahitimisho ya Brussels kuhusu uchunguzi uliofunguliwa dhidi ya Meta, X na makampuni mengine yatapatikana hivi karibuni.

Uchunguzi wa muda mrefu –

Ofisi yake imekosolewa barani Ulaya kwa kasi yake ndogo ya uchunguzi, huku wengine wakipendekeza ucheleweshaji huo ni wa makusudi, ili kuepusha kuleta shida na Ikulu ya White House.

Chunguzi kubwa kumi ztakamilika “katika wiki na miezi ijayo,” amejibu Henna Virkkunen.

Ili kuhalalisha kusubiri huku kwa muda mrefu, ameeleza kuwa mahitimisho yajayo yalikuwa ya kwanza kuchukuliwa chini ya DSA, “ndiyo maana timu za kisheria na kiufundi zilitaka kufanya kazi kwa uangalifu mkubwa na kuhakikisha kuwa kila mara tunakuwa na msingi thabiti wa kisheria tunapofanya maamuzi.”

Chunguzi hizo zinaweza kusababisha msukosuko wa kidiplomasia, lakini Virkkunen anaamini Marekani na EU bado zingenufaika kutokana na kufanya kazi kwa karibu zaidi juu ya sheria zinazosimamia teknolojia muhimu.

“Ushirikiano wa karibu utakuwa wa manufaa kwa pande zote mbili, kwa sababu kwa Marekani na makampuni katika sekta hiyo, EU ndilo soko kubwa zaidi la nje. Wengi wao wana watumiaji wengi zaidi katika Umoja wa Ulaya kuliko Marekani,” amebainisha.

Bi Virkkunen ametoa mfano wa Meta ambayo ina watumiaji wengi wa mtandao wake wa kijamii wa Instagram barani Ulaya kuliko Marekani.

“Ikiwa tutafanya kazi pamoja na Marekani, tunaweza kuweka kanuni na viwango katika kiwango cha kimataifa,” amesema. “Pia ingerahisisha shughuli za makampuni kote ulimwenguni.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *