Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya atoa indhari: Mustakabali wa EU uko ‘hatarini’

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya anayemaliza muda wake Josep Borrell ametoa indhari kuwa mustakabali wa umoja huo uko hatarini kutokana na kukabiliwa na migogoro mingi kwa wakati mmoja, na akasisitiza kwamba EU haiwezi tena kuitegemea Marekani kwa ajili ya ulinzi wake.

Borrell ametoa taswira inayotisha ya hali ya mambo duniani kwa mnasaba wa kuchapishwa majimui ya hotuba na makala zake zilizopewa jina la ‘Ulaya katika Tao la Moto.’ Ameorodhesha humo migogoro ya Ukraine, Ghaza na Afrika kuwa ni miongoni mwa masuala muhimu yanayotishia usalama wa dunia.

“Matukio ambayo tumelazimika kukumbana nayo katika miezi kadhaa iliyopita – kwa bahati mbaya – yamethibitisha utambuzi uliobainika mapema: Ulaya iko hatarini,” amesema Mkuu huyo wa Sera za Nje wa EU kupitia andiko aliloweka kwenye tovuti ya ofisi yake.

Borrel ameendelea kubainisha kwa kusema: “mazingira yetu ya kijiopolitiki yanazidi kuharibika, na mizozo na migogoro inazidi kuongezeka ikikaribia mlangoni kwetu. Kuanzia Ukraine hadi Mashariki ya Kati, kupitia Caucasus Kusini, hadi Pembe ya Afrika au Sahel. Yote haya yanajiri kinyume na matarajio, kutokana na kuzidi kuwa haina uhakika ahadi ya siku za usoni ya Marekani kuhusiana na usalama wa Ulaya”.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa EU amebainisha kwamba ahadi ya Washington “kwa usalama wa Ulaya kwa ujumla imekuwa isiyo na uhakika kwa siku zijazo,” kutokana na kuchaguliwa tena Donald Trump.

“Ustawi wetu na mustakabali wetu hauwezi kuendelea kutegemea vile wanavyohisi wapiga kura wa Marekani huko Midwest kila baada ya miaka minne,” ameeleza bayana Borrell huku akizitaka nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuimarisha ulinzi wao wenyewe…/