Mkutano wa Hali ya Hewa wa Umoja wa Mataifa (COP29) unendelea huko Baku nchini Azarbaijan, huku baadhi ya watu wenye ushawishi mkubwa duniani wakikwepa kuhudhuria, wakiwemo viongozi wa China, Marekani, India, Ujerumani na Ufaransa.
Kutokuwepo kwa viongozi wa nchi mbalimbali katika mkutano huo kumezua wasiwasi mkubwa miongoni mwa wanaharakati na jumbe zinazoshiriki, wakisema kuwa ni ishara ya kutowajibika kwa wazalishaji wakuu gesi chafu katika kushughulikia dharura ya hali ya hewa. Hata hivyo, wengi wanasema kwamba, udharura wa kushughulikia mgogoro wa hali ya hewa bado haujapungua, na juhudi za kimataifa lazima ziendelee na au bila watu hawo mashuhuri.
Katika hotuba yake ya leo Jumanne kwenye mkutano huo wa kila mwaka, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa ‘kutenda haki na uadilifu kwa hali ya hewa’.
Guterres amewaambia viongozi wa nchi mbalimbali waliokusanyika huko Baku kwamba suala la kuchukua hatua juu ya mabadiliko ya hali ya hewa halina mjadala na kwamba “wakati unayoyoma.”
“Kuhusu fedha za ufadhili wa hali ya hewa, dunia lazima ilipe, la sivyo ubinadamu utalipa gharama,” amesema Guterres na kuongeza kwamba: “Sauti unayosikia ni ya wakati unaoyoyoma. Tuko katika siku ya mwisho ya kuhesabu kupunguza joto duniani hadi nyuzi joto 1.5 na wakati hauko upande wetu.”

Mkutano wa sasa wa hali ya hewa (COP29) umepewa jina la “COP ya kifedha” kwa sababu unalenga kuongeza ufadhili ili kusaidia nchi za kipato cha chini katika kupunguza uzalishaji wa gesi chafu.
Ripoti inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imesema kuwa nchi zinazoinukia, ukiondoa Uchina, zinahitaji uwekezaji wa zaidi ya dola trilioni 2 kila mwaka ifikapo 2030 ili ulimwengu usitishe ongezeko la joto duniani.