Mkutano wa Kimataifa wa maswala ya bahari waanza Ufaransa

Kongamano hilo la tatu la Umoja wa Mataifa kuhusu Bahari limefunguliwa wakati shinikizo likiongezeka kwa mataifa kuzitekeleza ahadi zilizotolewa miongo mingi iliyopita za ulinzi wa kweli wa bahari.

Mkutano huo wa kilele unafanyika wakati ikibainika kuwa ni 2.7% tu ya bahari inayolindwa ipasavyo dhidi ya shughuli za uharibifu za uchimbaji. Hiyo ni kulingana na Taasisi isiyo ya faida ya Marine Conservation. Hiyo ni chini kabisa ya lengo lililokubaliwa chini ya ahadi ya kuhifadhi 30% ya ardhi na bahari ifikapo 2030. Ajenda kuu ya mwaka huu ni kupitishwa kwa Mkataba wa Ulinzi wa Bahari. Rebecca Hubbard ni Mkurugenzi wa Muungano wa Bahari. “Mkataba wa bahari ni muhimu ili kuhakikisha kwamba tunaweza kulinda viumbe hai katika bahari inayofunika nusu ya sayari. Hakuna sheria inayotupa uwezo huo na hivi sasa tuko katikati ya mzozo wa bioanuwai na tabianchina tunapaswa kulinda bahari ili kuweza kukabiliana na mizozo hiyo.”

Taka za plastiki zinahatarisha maisha ya viumbehai wa baharini
Utafiti wa Marine Conservation unaonyesha ni 2.7% tu ya bahari inayolindwa ipasavyo dhidi ya shughuli za uharibifu za uchimbajiPicha: Ocean Voyages Institute/ZUMAPRESS.com/picture alliance

Mkataba huo uliopitishwa mwaka wa 2023, kwa mara ya kwanza utaruhusu mataifa kuanzisha maeneo ya baharini yaliyohifadhiwa katika mipaka ya kimataifa, ambayo yanafikia karibu theluthi mbili ya bahari na kwa kiasi kikubwa hayatawaliwi.

Mkataba huo utaanza kutekelezwa mara tu nchi 60 zitakapouidhinisha. Kufikia Jumatatu, ni nchi 32 tu ndizo zilikuwa zimeridhia. Wanaharakati wanatumai kongamano hilo la UNOC linaweza kujenga kasi ya kutosha kufikiwa idadi hiyo na hivyo kuwezesha kupatikana kwa Mkataba huo.

Soma pia: Kongamano la kuokoa bahari lafunguliwa rasmi mjini Lisbon

Mtambo wa kukusanya taka jimboni California, Marekani
Juhudi zinafanywa na baadhi ya mataifa katika kusafisha fukwe za bahari zaoPicha: The Ocean Cleanup/AP/picture alliance

Korea Kusini, Ufaransa na Umoja wa Ulaya zimepigania mkataba huo, lakini mataifa mengi makubwa yenye bahari bado hayajaidhinisha, ikiwa ni pamoja na mataifa mengine ya Kundi la G20. Maelfu ya wajumbe wanatarajiwa mjini Nice _ kuanzia wajumbe wa kawaida na wakuu wa nchi hadi wanasayansi na viongozi wa sekta hiyo. Marekani bado haijathibitisha ujumbe rasmi.

Mkutano huo utajumuisha majopo 10 yatakayojadili mada kama vile uchumi wa bluu, uvuvi endelevu na uchafuzi wa bahari kutokana na taka za plastiki. Uchimbaji madini wa baharini unatarajiwa kujitokeza katika mijadala mipana, wakati mataifa ya visiwa vidogo yana uwezekano wa kutumia jukwaa hilo kutetea kuongezwa kwa ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Matokeo ya kongamano hilo la siku tano yataunda msingi wa kile kinachojulikana kama Mpango Kazi wa Niece kuhusu Bahari _ ambao ni tamko la ahadi za hiari zitakazopitishwa kwa makubaliano na kuwasilishwa kwenye Umoja wa Mataifa huko New York Julai mwaka huu.

DPA/AP

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *