
Mkutano huo wa kilele wa kila mwaka wa wakuu wa nchi na serikali za Umoja wa Afrika, AU, unaanza siku ya Ijuma na utatanguliwa na vikao kadhaa vya awali.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Viongozi wa nchi za Afrika waliwasiili jijini Addis siku ya Alhamisi kwa kikao maalum cha umoja huo ambapo tamko la pamoja kuhusu hali mashariki mwa DRC litatolewa na baadaye kushiriki kura za uenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika.
Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika litakutana kwa kikao maalumu cha kuujadili mzozo wa Kongo, ambako waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wamechukua udhibiti wa maeneo kadhaa upande wa mashariki wenye utajiri mkubwa wa madini.
Umoja wa Afrika umesema viongozi wote wakuu watashiriki mkutano huo wa Baraza la Usalama. Hata hivyo serikali ya Kongo imesema Rais Felix Tshisekedi hatoshiriki kikao hicho cha leo na badala yake amemtuma waziri wake mkuu Judith Suminwa Tuluka.
Ofisi ya Tshisekedi imesema kiongozi huyo yuko mjini Munich kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa usalama na atakwenda Addis mnamo Jumamosi kwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika.
Hadi sasa bado haijafahamika pia kama Rais Paul Kagame wa Rwanda atahudhuria kikao cha leo kitakachoijadili Kongo. Serikali yake inanyooshewa kidole kwa kuwasaidia wapiganaji wa M23.
Shirika la kimataifa inayoshughulikia mizozo, ICG, imesema mzozo wa Kongo unatishia “kugeuka chanzo cha makabiliano baina ya mataifa mengi ya kanda ya maziwa makuu na kukumbusha mifarakano iliyogubika kanda hiyo miaka ya 1990”.
Wiki iliyopita jumuiya mbili za kikanda ile ya SADC na nchi za Afrika Mashariki zilifanya mkutano wa pamoja kuhusu Kongo mjini Dar es Salaam.
Tamko lao la pamoja lilitaka mapigano yasitishwe na kuishinikiza serikali ya Kongo kufanya mazungumzo na makundi ya waasi ikiwemo M23.
Serikaliya Kongo imekataa mara kadhaa kufanya mkutano na kundi la waasi la M23, likilitaja kwamba ni kundi la kigaidi.