
Wakuu wa nchi za Afrika wanakutana mwishoni mwa juma hili mjini Addis Ababa kwa ajili ya mkutano wa kila mwaka wa Umoja wa Afrika (AU) ambao utamteua mwenyekiti mpya wa tume ya umoja huo, katikati ya mzozo unaoendelea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Imechapishwa:
Dakika 3
Matangazo ya kibiashara
Mashariki mwa DRC, kundi la waasi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda lilichukua udhibiti wa Goma, mji mkuu wamkoa wa Kivu Kaskazini, mwishoni mwa mwezi wa Januari kabla ya kusonga mbele kuelekea mkoa jirani wa Kivu Kusini. Kinyume chake, jeshi la Kongo linaungwa mkono haswa na wanajeshi wa Afrika Kusini na Burundi.
Mgogoro huo unaongeza orodha ndefu ya changamoto zinazoikabili AU, shiŕika linalowakilisha kaŕibu Waafŕika bilioni 1.5, lenye makao yake makuu mjini Addis Ababa na kukosolewa mara kwa mara kwa uzembe wake na misimamo ya woga.
Tangu kuongezeka kwa mzozo wa hivi majuzi, na wakati Kinshasa imekuwa ikitoa wito kwa vikwazo vya kimataifa dhidi ya Kigali bila mafanikio, wito kutoka kwa jumuiya ya kimataifa wa kusitishwa na usitishaji mapigano umeongezeka, huku baadhi ya nchi na Umoja wa Mataifa pia zikitoa wito wa kuondolewa kwa wanajeshi wa Rwanda mashariki mwa DRC.
AU pia ilitoa wito wa kusitisha mapigano, lakini bila kuitaja Rwanda.
“Hatari kwamba vita hivi vinaweza kugeuka kuwa makabiliano kati ya nchi kadhaa katika eneo la Maziwa Makuu vikikumbushaa maovu ya miaka ya 1990 ni kubwa,” Shirika la Kimataifa linalotatua migogoro International Crisi Group (ICG) linaonya katika ripoti.
Hali “mbaya”
Mapigano ya hivi majuzi mashariki mwa Kongo, ambayo imekumbwa na ghasia kwa miaka 30, yamesababisha vifo vya watu 2,900 kulingana na Umoja wa Mataifa.
Katika hali hii “ya maafa”, AU “ina uwezo wa kuwa mstari wa mbele katika mazungumzo ya amani na kuweka shinikizo kwa kila upande ili kuepuka ongezeko jipya la uhasama,” anabainii Liesl Louw-Vaudran, mtafiti katika ICG na mtaalamu katika AU.
DRC itakuwa kwenye ajenda ya mkutano wa wakuu wa nchi za bara hilo uliopangwa kufanyika siku ya Ijumaa, kabla ya mkutano rasmi wa kilele Jumamosi na Jumapili, amesema Paschal Chem-Langhee, mratibu anayehusika na mawasiliano wa Baraza la Amani na Usalama la AU (PSC).
Hakutaja kama mkuu wa nchi ya Kongo Félix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame watahudhuria pamoja ana kwa ana.
Rais wa Angola Joao Lourenço, ambaye amekuwa akihusika pakubwa katika majaribio ya upatanishi kati ya DRC na Rwanda kwa miaka kadhaa, atachukua urais wa zamu wa AU mwishoni mwa juma hili, jukumu la kiheshima.
Mwishoni mwa mkutano huo, mwenyekiti mpya wa Tume ya AU atateuliwa kumrithi Moussa Faki Mahamat, raia wa Chad, ambaye amefikia kikomo cha mihula miwili ya jukumu hili la utendaji.
Wagombea watatu wanawania wadhifa huo, wakati huu nafasi hii ikitengewa mwakilishi kutoka Afrika Mashariki: Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti Mahmoud Ali Youssouf, mkongwe wa upinzani wa Kenya Raila Odinga na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar Richard Randriamandrato.
“Kuna vigezo vingi kiasi kwamba haiwezekani kusema nani atashinda uchaguzi,” Benjamin Augé, mtafiti katika kituo cha Afrika cha Taasisi ya Uhusiano ya Kimataifa ya Ufaransa (Ifri), amelieleza shirika la habari la AFP.
“Viongozi wengi wa Afrika wameahidi hadharani kumuunga mkono Raila Odinga lakini kura ndio itakayoamua” anaongeza Liesl Louw-Vaudran.
Uchaguzi huo unafanywa na thuluthi mbili ya wingi wa nchi wanachama zilizo na haki ya kupiga kura, ambazo hazijumuishi nchi sita ambazo zimesimamishwa kwa sasa kufuatia mapinduzi ya kijeshi, kama vile Gabon, Mali na Niger.