Mkutano mkuu Chaumma na sura za G55

Dar es Salaam. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma),  kinafanya vikao viwili cha kamati kuu na halmashauri kuu, ambapo mbali ya kuhudhuriwa na makada wa chama hicho, wapo pia waliojiengua Chadema.

Mwananchi Digital ilipofika katika eneo vinakofanyika vikao hivyo, mbali na wajumbe waliovalia sare za Chaumma, katika kikao hicho, wameshuhudiwa baadhi ya waliokuwa makamanda wa Chadema, akiwemo mlinzi binafsi wa Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Freeman Mbowe.

Magari mbalimbali yaliyobeba wajumbe yanaendelea kuingia katika eneo hilo.

Hata hivyo, baadhi ya makada hao, wamesema wanajua kunakwenda kufanyika kikao cha Kamati Kuu na Halmashauri Kuu, lakini hawana taarifa ya ajenda zitakazojadiliwa.

“Tunajua kuna wanachama kutoka Chadema wanajiunga, hatuna uhakika ni kina nani lakini tunalijua hilo,” amesema mmoja wa jumbe hao kwa sharti la kutotajwa jina, huku akiongeza kuwa ujio wa wanachama hao ni furaha kwa chama ila hawajui kama watakuwa na faida kwao au laa.

Ukiacha walinzi waliokuwa wa Chadema, pia aliyegombea uenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema Taifa (Bavicha), Masoud Masoud alikuwa miongoni mwa vijana waliokuwepo eneo hilo.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bawacha Mbagala, Khadija Mwago naye alikuwa sehemu ya waliokuwepo katika eneo hilo, akifanya mazungumzo na makada mbalimbali wa Chaumma.

Pamoja naye, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Kinondoni, Henry Kilewo hilo akipiga stori za hapa na pale na wajumbe wa vikao hivyo.

Pirikapirika zilianza asubuhi ambapo makada na viongozi wa Chaumma, walikutana makao makuu ya chama hicho, Makumbusho jijini Dar es Salaam, tayari kuhudhuria vikao vya  Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya chama hicho, inayofanyika leo, Jumatatu, Mei 19, 2025 kisha utafuatia mkutano mkuu utakaofanyika Jumatano ya wiki hii.

Tangu saa 1:00 asubuhi wajumbe walishafika ziliko ofisi za makao makuu ya chama hicho Makumbusho jijini Dar es Salaam, kuchukua sare kisha kuanza utaratibu wa kwenda eneo la mkutano.

Baadhi ya wajumbe waliofika katika ofisi hizo kuchukua sare ni viongozi wa chama hicho ngazi ya mikoa, wilaya na Taifa, huku Mwenyekiti, Hashim Rungwe akiwasili saa 2:58 asubuhi.

Ukiacha pilika za huku na kule za viongozi, kila mjumbe alivalia fulana zenye rangi nyekundu na nembo ya chama hicho, huku Rungwe akiongezea na koti la suti la buluu juu ya fulana yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *