
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Jatu PLC, Peter Gasaya (33), anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashitaka mawili likiwamo la kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu, amefikisha siku 690 akiwa gerezani kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokamilika.
Mbali na upelelezi kutokamilika, mshtakiwa huyo kupitia wakili wake, Nafikile Mwamboma ameiomba Mahakama hiyo imfutie kesi mteja wake na imuachie huru.
Gasaya anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka katika Saccos ya Jatu kwa madai kuwa fedha hizo atazipanda kwenye kilimo cha mazao ili kuzalisha faida zaidi, wakati akijua kuwa ni uongo.
Kwa mara ya kwanza, Gasaya alifikishwa mahakamani hapo Desemba 29, 2022 na kusomewa mashitaka yanayomkabili.
Hata hivyo, tangu afikishwe mahakamani hapo hadi leo Jumatatu Novemba 18, 2024 amefikishwa siku 690, sawa na mwaka mmoja, miezi 10 na siku 20 akiwa gerezani kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokukamilika.
Wakati mshtakiwa akifikisha siku hizo bila upelelezi kukamilika, upande wa mashitaka umedai kuwa bado unaendelea na upelelezi wa shauri hilo.
Wakili Roida Mwakanyamale ameieleza Mahakama hiyo mbele ya hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini, kuwa shauri hilo limeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado unaendelea.
Baada ya kueleza hayo, wakili wa mshtakiwa, Nafikile Mwamboma ameomba Mahakama imfutie kesi mteja wake kutokana na shauri hilo kufutwa na kufunguliwa upya, bila upelelezi kukamilika.
“Mheshimiwa hakimu, Mahakama yako ina mamlaka ya kudhibiti mwenendo wa kesi zake, na hii kesi ilishafutwa na kufunguliwa mara ya pili, nilitegemea upelelezi ungekamilika kwa wakati ili iendelee na hatua nyingine, lakini kutokana na upelelezi kutokamilika naiomba Mahakama yako imfutie kesi mteja wangu na imwachie huru” amedai Mwamboma.
Baada ya kueleza hayo, hakimu Mhini aliutaka upande wa mashitaka kuhakikisha wanakamilisha haraka upelelezi wa shauri hilo na kisha kuahirisha kesi hiyo hadi Desemba 2, 2024 kwa ajili ya kutajwa.
Tofauti na siku nyingine ambapo kesi huendeshwa kwa njia ya video, leo mshtakiwa huyo ameletwa mahakamani kwa ajili ya kesi yake kutajwa.
Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anakabiliwa na mashitaka mawili ambayo ni kujipatia kiasi hicho cha fedha pamoja na kutakatisha Sh5.1bilioni katika kesi ya uhujumu uchumi namba 8/2023.
Katika shitaka la kwanza, mshtakiwa anadaiwa, katika ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es Salaam, akiwa kama Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh5,139,865,733 kutoka Saccos ya Jatu.
Alieleza kuwa fedha hizo ataziingiza kwenye kilimo jambo ambalo alijua kuwa sio kweli.
Shitaka la pili ni kutakatisha kiasi hicho cha fedha tukio analodaiwa kulitenda kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es salaam.
Siku hiyo ya tukio na eneo hilo, mshitakiwa akiwa Mtendaji Mkuu na mwanzilishi wa Jatu saccos, alijihusisha na muamala wa Sh5,139,865,733 kutoka katika akaunti ya Jatu saccos iliyopo benki ya MNB tawi la Temeke, kwenda katika akaunti ya Jatu PLC iliyopo katika benki ya NMB tawi la Temeke, wakati akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.