Dar es Salaam. Baada ya ukimya wa takriban miezi minne, Meneja wa msanii wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’, Said Fella ‘Mkubwa Fella’ aliyeelezwa anaumwa, ameibuka na kuvunja ukimya kuhusu afya yake.
Taarifa za kuumwa kwake ziliibuka kwenye mitandao ya kijamii amepoza miguu huku wengi wakidai Diamond amemtelekeza.
Stori zilizidi, Fella anaumwa na hataki watu waende kumwona kutokana na hali yake na anaongea kwa tabu.
Ili kujua ukweli wa stori hizi, Desemba 31, 2024, Mwananchi ilimtafuata nyumbani kwake Kilungule jijini Dar es Salaam na mwandishi alipokewa na watoto wake na wengine walidai yupo ndani anaumwa na wengine wakidaii ametoka.
Mtoto wake wa kiume alisema “Baba yuko ndani” wakaribie ndani.
Hata hivyo, baada ya kuingia ndani ya geti mtoto mwingine wa kiume aliyedai asubirie anakuja, huku dada aliyekuja aliko mwandishi alisema Fella hayupo ametoka, kabla ya mtu mmoja aliyejitambulisha kama ndugu wa Fella kusema anaumwa hivyo amepumzika hataki heka heka za watu.

Februari 3, 2025, Mwananchi ilimrudia tena kufahamu hali yake na kwa njia ya simu, mwandishi alimpigia na alifunguka kwa kifupi.
“Mimi naumwa bana, ila kwa sasa naendelea vizuri kidogo tofauti na mwanzo nilivyokuwa, nashukuru Mungu sijambo,” alisema Mkubwa Fella huku akisita kutaja kinachomsumbua.
Hata hivyo, kabla ya Mwananchi kwenda nyumbani kwake, iliwasiliana na ndugu yake anayejulikana kwa jina la Said na kusema ni kweli Fella anaumwa.
“Bwana mkubwa Fella anaumwa kweli, japo vipo vitu nyuma ya pazia ambavyo ukikutana naye wewe mwenyewe kwa kuwa mnafahamiana ataamua kukwambia, ila alianza kuumwa na presha iliyosababisha kupooza upande mmoja na hata watu wanaosema Diamond hamsaidii sio kweli.”
“Diamond yupo naye bega kwa bega tangu alipoanza kuumwa akapelekwa Hospitali ya Mlogamzila, kafaulishwa Muhimbili na baada ya hapo akapelekwa Hospitali ya TM, hapa akaanza kupata unafuu kwa mbali ndipo akapelekwa India kwa ajili ya matibabu ya mwezi mzima,” anasema Said.

Mwananchi ilimtafuta Babu Tale ambaye ni mtu wa karibu wa Fella na kukiri anaumwa.
“Ni kweli anaumwa na kuumwa ni ibada na ugonjwa siyo kumtangazia kila mtu, kwa nini wafanye matangazo? Labda kama mhusika anahitaji kufanya hivyo sawa atafanya, lakini kusema anaumwa kimya kimya sijaona sababu ya kuwatangazia watu na Fella kwa sasa anaendelea vizuri, anapata sapoti kwetu na Diamond pia,” alisema Babu Tale.