
Unguja. Wakati mke wa Rais wa Finland Suzanne Innes-Stubb akizindua jengo la dawati la jinsia na watoto Zanzibar na kutajwa kuwa kimbilio la wengi, takwimu za miaka mitatu za ukatili wa kijinsia zimefikia 107,260 nchini.
Akizungumza wakati wa kuzindua jengo hilo leo Mei 15, 2025, Kamishana wa Polisi jamii Tanzania, Faustine Shilogile amesema takwimu hizo ni za kuanzia mwaka 2022 ambapo yalikuwa makosa, 32 566, mwaka 2023, makosa 37,448 na mwaka 2024 makosa 39,256 huku akitaka jamii kuendelea kutoa taarifa kwani wanapokaa kimya ni sehemu ya kuchangia matukio hayo yaendelee kutokea.
Fedha za jengo hilo zilitolewa na Serikali ya Finland kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (NFPA) kwa kushirikiana na TGNP. Hata hivyo gharama za mradi huo unaojumuisha na majengo mengine Tanzania bara, hazikutajwa.
Kwa upande wa Zanzibar pekee kwa kipindi hicho, amesema kulikuwa na matukio 4,205 kati ya hayo makosa ya kubaka 2047, kulawiti 603, kuingilia kinyume na maumbile 49, kutorosha watoto 332 na shambulio la aibu makosa 644.
“Haya matukio yalitokea katika Mkoa wa Mjini Magharibi na wilaya zake zote na ikifuatiwa na Kaskazini Unguja, Kusini Unguja na Pemba,” amesema.
Amesema matukio hayo yameibuka kipindi cha hivi karibuni ambapo hayakuwapo awali na waathirika wakuu ni watoto na wanawake hivyo hayapaswi kufumbiwa macho na kila mmoja atoe sauti kwa maana ya viongozi wote wa dini, wanasiasa na wazee kupinga na kukemea vitendo hivyo.
Amesema kwa muda mrefu ukatili wa kijinsia umekuwa ukihusisha wanawake wakiwa waathirika wakuu lakini hata wanaume ni waathirika wa matukio hayo na mara nyingi wamekuwa wakikaa kimya kwa kuogopa aibu kwenye jamii.
“Ukijua unanyanyaswa sema, wapo wanaume wengi wanapata ukatili lakini hawasemi, ukjiua ukatili halafu ukashindwa kusema wewe ni miongoni mwa wanaouchangia,” amesema.
Naye Mke wa Rais wa Finland, Suzanne amesema Serikali za Tanzania na Finland zimekuwa marafiki na wamejiunga kuhakikisha wanaleta maendeleo katika Taifa ikiwamo kuinua haki za wanawake na wasichana.
Amesema wanaamini Taifa lolote ambalo litakuwa na maendeleo halipaswi kuwa na vitendo vya ukatili wa wanawake na wasishana, akisema kumwezesha msichana ni sehemu ya haki za binadamu.
“Mwanamke ndio mlezi wa jamii kwa hiyo inapokuwa hakuna unyanyasaji hata maendeleo ni rahisi kupatikana, kwa hiyo Finland itaendelea kushirikiana na Tanzania katika harakati zake za kupambana na vitendo hivi,” amesema.
Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi (UNFPA), Mark Brayan amesema kuwapo kwa dawati la jinsia ni dhahiri kila mmoja atapata haki yake bila kujali ni watu wa aina gani.
Amesema huo ni mpango kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika kushughulikia haki za binadamu.