Mke aliyemkodi kaka yake kumuua mumewe kwa Sh100,000, kunyongwa

Arusha. Watu watatu wamehukumiwa adhabu ya kifo, akiwamo mke aliyemkodi kaka yake na mtu mwingine kisha kuwalipa Sh100,000 ili wamuue mumewe kwa madai alikuwa akifuja mali ya familia kwa kuuza vyakula na kwenda kunywa pombe.

Mshtakiwa huyo wa kwanza, Rehema Maksoni alimkodi kaka yake, Ajuaye Maksoni na Shadrack Paschal ambao walimchoma mumewe Lameck Makupi na kitu chenye ncha kali tumboni kilichosababisha utumbo mkubwa kutoka.

Ilidaiwa mahakamani hapo Rehema alipokamatwa na kuhojiwa alikiri kupanga mauaji ya mumewe akidai alikuwa akifuja mali ya familia kwa kuuza vyakula na kutumia fedha hizo kunywa pombe hivyo alimchoka.

Hukumu hiyo imetolewa jana Jumatatu Septemba 23, 2024 na Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma mbele ya Jaji John Nkwabi, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo.

Ilivyokuwa

Katika utetezi wake mahakamani hapo, Rehema alidai Februari 23, 2023, mume wake alichukuliwa nyumbani na kundi la wanaume watano, wanne kati yao wakiwa wamevalia sare za polisi huku kati yao wawili wakiwa na silaha.

Alidai mlango ulipogongwa, alijibu hodi, alipofungua alikutana na kaka wa marehemu, Gideon Makupi akiwa na askari hao wanne waliokuwa wakimtaka mumewe ambaye kwa wakati huo alikuwa amelala.

Alidai alikwenda kumwita mumewe na alipotoka nje alipandishwa kwenye gari na kuondoka naye.

Asubuhi ya siku iliyofuata, dereva wa lori aliyekuwa akipita katika Kijiji cha Samvura, aliona mwili wa mtu ukiwa umelala kando ya barabara na kutoa taarifa kwa shahidi wa tatu aliyetajwa kwa jina la Ladislaus.

Ilidaiwa katika eneo hilo, mwili huo ulikutwa kando ya barabara na baadaye daktari alithibitisha mtu huyo amefariki dunia.

Baada ya mwili huo kukutwa, Rehema alikamatwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mumewe na kudaiwa kukiri wakati anahojiwa na polisi.

Ilidaiwa baada ya kuwa na nia hiyo ya kumuua mumewe, aliomba ushauri na usaidizi kwa Sh100,000 maelezo anayodaiwa kukiri pia mbele ya Hakimu wa Amani, Sophia Timtenge (shahidi wa tano wa mashtaka).

Shahidi huyo wa tano, aliyerekodi maelezo hayo ya ziada, yalipokewa mahakamani kama kielelezo bila pingamizi kutoka kwa wakili wa utetezi huku akisisitiza maelezo hayo yamechukuliwa kwa mujibu wa sheria.

Daktari aliyefanyia uchunguzi mwili huo alidai Lameck alifariki dunia kutokana na upungufu wa damu kwenye ubongo na kuvuja damu nyingi kwani tumbo lilikuwa limechomwa na kitu chenye ncha kali.

Awali, Rehema alikiri mbele ya shahidi wa saba  Koplo Felix, kuwa aliomba msaada kwa mshitakiwa wa tatu (kaka yake) ambaye naye aliomba msaada kwa mshtakiwa wa pili (Shadrack).

Shahidi wa tisa, Moran Enos alidai polisi walimkamata Shadrack Mtaa wa Malagarasi mjini Kibondo, ambaye alifanikisha kukamatwa kwa Ajuaye; na kisu kilichodaiwa kutumika kwa mauaji hayo kilikamatwa katika chumba cha kupanga cha Shadrack.

Washitakiwa hao katika utetezi wao walipinga kutenda kosa hilo la mauaji kinyume na vifungu tajwa hapo juu na kukanusha kurekodi maelezo yoyote ya onyo na kudai waliteswa na kutishiwa.

Akijitetea mahakamani hapo, Rehema alikana kupanga mauaji ya mume wake na kudai alikuwa na uhakika alipochukuliwa usiku alipelekwa kituo cha polisi kwa madai haikuwa mara yake ya kwanza kupelekwa kituo cha polisi.

Zaidi ya hayo, alidai shemeji yake (Gideon), alimsisitiza kubaki nyumbani kwani kila kitu kitakuwa sawa na marehemu, huku Shadrack akidai kukamatwa akiwa chumbani kwake na kukana kutenda kosa hilo.

Mshtakiwa wa tatu (Ajuaye), alipinga kutenda kosa hilo na kudai usiku wa kuamkia siku hiyo alikuwa Kasulu Mjini akiwa anajishughulisha na usambazaji wa bidhaa katika vijiji mbalimbali vya wilaya hiyo.

Katika uamuzi wake ambao nakala yake inapatikana katika mtandao wa Mahakama, Jaji Nkwabi amesema Mahakama inazingatia masuala mawili katika kuamua kesi hiyo iwapo watuhumiwa hao walimuua Lameck.

Suala la pili na Mahakama inaangalia kama watuhumiwa walikuwa na nia mbaya ya mauaji na kuwa amezingatia kwa umakini ushahidi wa pande zote mbili na kuwa washtakiwa hao walimuua marehemu.

Jaji amesema kwa kuanza na mshtakiwa wa kwanza (Rehema), ambaye alipohojiwa alikiri walipanga njama za kumuua mumewe na kuwalipa Sh100,000 ila katika utetezi wake alidai polisi ndiyo wanapaswa kulaumiwa kwa kumchukua mumewe wakiwa na shemeji yake.

Jaji huyo amesema anakataa utetezi huo wa Rehema na kuwa msimamo wake unatokana na msimamo wa Mahakama ya Rufani katika kesi ya Damian Ferdnand Kiula na Charles dhidi ya Jamhuri ya mwaka 1992 ambayo ilielezwa:

“Kwa upande wetu hatufikirii kulikuwa na sababu za msingi za kuzingatia tamko la kufa katika kielelezo cha pili kuwa dhaifu na lisilotegemewa. Ilirekodiwa na ofisa wa polisi ambaye hakuwa na sababu ya kusema uwongo dhidi ya mrufani.”

“Kwa maoni yangu, nikikubali utetezi wa mshitakiwa wa kwanza ambaye hakumuita Gideon kama shahidi wake wa utetezi utaiacha jamii ikijiuliza, kwa nini sheria imetengana kwa akili ya kawaida? Ikiwa ni kweli, Gideon alikuwa na maofisa wa polisi walipokuja kumkamata marehemu, angependa kumtetea shemeji yake,” amesema.

Jaji ameeleza polisi hawakusema marehemu alikuwa mhalifu na wasingeweza kumdhuru raia asiye na silaha na kuwa ana uhakika iwapo marehemu angeuawa na wanaodaiwa kuwa ni polisi, Gideon asingepumzika mpaka apate haki kwa ndugu yake aliyeuawa.

“Haishangazi kwamba hakuja kutoa ushahidi mahakamani ili kuunga mkono utetezi wa shemeji yake. Kama ilivyokuwa kwa Kiula (supra) sioni sababu yoyote kwa nini polisi wangemhusisha mshitakiwa wa kwanza bila sababu,” amefafanua Jaji.

Huku akinukuu kesi mbalimbali zilizowahi kuamuliwa na Mahakama ya Rufani, Jaji Nkwabi amesema katika kesi hiyo mshtakiwa wa kwanza alikiri mbele ya Hakimu wa Amani na ameridhika kwamba maelezo yake ya ziada ya ungamo, ni ya kweli na anashikilia kuwa alipanga njama ya kumuua mumewe.

“Ikumbukwe ingawa mshtakiwa wa kwanza hakwenda kwenye eneo ambalo marehemu alikutana na kifo chake wakati huo, anawajibika kwa kifo chake,” amesema.

Kuhusu mshtakiwa wa tatu (Ajuaye), Jaji Nkwambi amesema amejadili kwa kirefu umuhimu wa taarifa za nje ya Mahakama na maelezo ya ziada ya mshtakiwa huyo yanatosha kumtia hatiani.

Kuhusu hoja ya kukamatwa kwa kisu kunathibitisha kesi ya mashtaka dhidi ya mshtakiwa wa pili (Shadrack), Jaji amesema kwa maoni yake mshtakiwa huyo alipaswa kuripoti kwa polisi ikiwa hakuwa sehemu ya njama ya kumuua marehemu.

Jaji amesema Shadrack ambaye pia alikiri mbele ya Hakimu wa Amani kuwa alikiri kupokea fedha Sh40,000 na kumlipa bodaboda Sh10,000;  kwa nini alilipwa Sh 40,000 kama hakuwa mkosaji, hivyo anashikia kuwa mshitakiwa huyo alimuua marehemu.

Baada ya kuchambua ushahidi wa pande hizo, Jaji Nkwabi amesema washitakiwa wote walikuwa na nia mbaya ya mauaji hivyo anawatia hatiani kwa mauaji kama walivyoshitakiwa.

“Washtakiwa hao walimchoma marehemu tumboni, sehemu ambayo ni hatari kwa mwili, sababu ya kuuawa ni kwamba marehemu alimuudhi mshtakiwa wa kwanza kwa kufuja mali za familia,hivyo alitaka kumuondoa na ndivyo ilivyofanyika,” amesema Jaji.

“Uovu uliofikiriwa hapo awali uko wazi katika kesi hii, majadilianao ya hapo juu yanathibitisha wazi watuhumiwa walikuwa na nia ya kumuua marehemu. Kwa hiyo nawaona washtakiwa wana hatia ya mauaji na adhabu ni moja tu kwa kosa la kuua yaani adhabu ya kunyongwa,” amehitimisha Jaji.