Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesaini makubaliano na Jamhuri ya Czech ya kuepuka kodi ya mara mbili, hatua inayolenga kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI) na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.
Mwaka 2022, biashara baina ya mataifa hayo iliongezeka hasa katika sekta za huduma, mashine, vifaa vya umeme, usafiri na teknolojia.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD), nchi zilizo na mikataba madhubuti ya aina hiyo hupokea hadi asilimia 30 zaidi ya uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje ya nchi ikilinganishwa na zile zisizo na mikataba hiyo.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Mei 14, 2025 na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa kodi ya mara mbili baina ya Tanzania na Jamhuri ya Czech iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Dk Nchemba amesema makubaliano hayo ni hatua ya kihistoria inayolenga kuondoa urasimu katika masuala ya ushuru, kulinda faida za wawekezaji na kukuza mazingira rafiki ya biashara.
“Kuepuka kodi ya mara mbili si suala la kiufundi tu bali ni chombo madhubuti cha kujenga imani kwa wawekezaji, kulinda faida zao, na kuhimiza uamuzi wa haki katika sera za kodi,” amesema Dk Nchemba.
Amesema mafanikio ya kufikiwa kwa makubaliano hayo yametokana na uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameendelea kuandaa mazingira rafiki kwa wawekezaji kupitia mageuzi ya sera na mifumo ya kodi.
“Serikali imefanya mageuzi makubwa kama kurahisisha usajili wa biashara, utoaji wa leseni, pamoja na kuweka mifumo ya kidigitali ya ukusanyaji wa kodi na ushuru. Haya yote yamelenga kuvutia wawekezaji zaidi na kufanya Tanzania kuwa kivutio kikuu cha uwekezaji,” amesema.

Amesema Tanzania inatajwa kuwa miongoni mwa nchi tatu zinazoongoza kwa kuvutia uwekezaji Kusini mwa Jangwa la Sahara, nyuma ya Afrika Kusini na Nigeria. Uchumi wake unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia sita kufikia mwisho wa mwaka 2025.
“Makubaliano haya ni mwanzo muhimu kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Czech kuchangamkia fursa zilizopo. Natoa wito kwa taasisi za serikali na mamlaka za kodi kuhakikisha makubaliano haya yanatekelezwa kwa uwazi na kwa ufanisi,” amesisitiza.
Makubaliano hayo amesema yanatarajiwa kusaidia Tanzania kunufaika na soko la zaidi ya watu milioni 400 katika ukanda wa Afrika Mashariki huku nchi hiyo ikitajwa kuwa lango kuu la kibiashara katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Balozi wa Jamhuri ya Czech nchini Tanzania, Nicol Adamcova amesema makubaliano hayo ni uthibitisho wa kuaminiana kwa kiwango cha juu kati ya nchi hizo, jambo ambalo lingewezekana tu kwa kutumia muda na nguvu kubwa kwenye mazungumzo.
“Makubaliano haya si tu kwamba yanaondoa vikwazo vya kodi, bali pia ni ishara ya utulivu wa mazingira ya biashara Tanzania na Czech,” amesema Adamcova.
Katika kuimarisha ushirikiano, Balozi huyo amesema yeye pamoja na timu yake wanatarajiwa kusafiri kwa treni ya SGR kuelekea Morogoro, ambapo watatembelea kiwanda cha kutengeneza ndege kidogo kinachoitwa Airplanes Africa Limited (AAL) mradi wa ubia kati ya Tanzania na Czech katika sekta ya anga.
“Kutengeneza ndege si jambo rahisi, hii ni hatua ya kujivunia na inaonyesha uwezo wa ushirikiano wa kiteknolojia kati ya nchi zetu mbili,” amesema.
Aidha, ameeleza kuwa injini za umeme zinazotumika katika treni ya SGR zimetengenezwa na kampuni ya Czech, jambo ambalo linaonyesha ushirikiano wa muda mrefu katika sekta ya miundombinu.
Pia, ameeleza matarajio ya kuimarika kwa ushirikiano wa pande zote mbili hususani kwenye sekta za teknolojia, afya, elimu na utafiti.
Mbali na hayo, Adamcova ametoa salamu za pole kwa Serikali na wananchi kufuatia kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya aliyefariki dunia Mei 7, 2025 katika hHspitali ya Mzena kwa maradhi ya moyo.