Mkasa wa dakika 10 za Dele Alli Como

Milan, Italia. Staa wa timu ya Como, Dele Alli jana aliweka rekodi na kupewa kadi nyekundu dakika kumi tu baada ya kurejea uwanjani.

Alli ambaye ni staa wa zamani wa Tottenham Hotspur alikuwa amekaa nje kwa zaidi ya miaka miwili lakini aliporejea tu amekutana na kadi hiyo.

Nyota huyo amekuwa nje kwa muda mrefu akiwa anasumbuliwa na majeraha na aliporejea kwenye mchezo wake wa kwanza ndani ya kikosi cha Como akakutana na kadhia hiyo.

Alli alijiunga na Como kwenye dirisha kubwa la usajili na alikuwa hajatumika kwenye timu hiyo kwa kipindi chote alichokuwa na timu hiyo.

Kocha wake Cesc Fabregas alishasema tangu juzi kuwa anataka kumtumia mchezaji huyo kwa kuwa anaona anaweza kuisaidia timu yake, lakini zilimtosha dakika hizo tu kwenye mechi hiyo dhidi ya AC Milan.

Kabla ya mchezo huu, Alli alikuwa amecheza mechi ya mwisho Februari 2023 ambapo aliitumikia Besiktas ilipotoka suluhu na Antalyaspor.

Staa huyo alimchezea madhambi Ruben Loftus-Cheek, mwamuzi akamuonyesha kadi ya njano, lakini marudio ya VAR yaliamua kuwa mchezaji huyo anatakiwa kupewa kadi nyekundu katika dakika ya 89 zikiwa ni kumi tangu aingie akitokea benchi.

Hata hivyo, wakati anapewa kadi hiyo tayari timu yake ilikuwa nyuma kwa mabao 2-1 yaliyofungwa na Chrstian Pulisic na Tijjan Reijnderes, huku lile la Como ambayo ipo nafasi ya 13 kwenye msimamo likiwekwa kimiani na Lucas da Cunha.

Dakika mbili baada ya Alli kupewa nyekundu kocha wake Fabregas naye alipewa kadi ya pili ya njano kutokana na malalamiko yake kwa mwamuzi wa mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Giussepe Meanza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *