Mkakati wa Israel: Mashambulizi hafifu, kukuza na kutia chumvi kwenye vyombo vya habari

Wakati utawala wa Kizayuni wa Israel ukidai kuwa umeshambulia maeneo 20 nchini Iran, wachambuzi wa mambo wanasema kuwa shambulio hilo lililofanyika mapema leo halilingani hata kidogo na Opereshen Ahadi ya Kweli-2 (Operation ‘True Promise 2) iliyotekelezwa na Iran dhidi ya utawala huo katili majuma kadhaa yaliyopita.

Asubuhi ya leo (Jumamosi), tarehe 26 Oktoba, msemaji wa utawala wa Kizayuni wa Israel ametangaza kuwa utawala huo ghasibu umeshambulia maeneo ya kijeshi nchini Iran kujibu mashambulizi ya mara kwa mara ya Iran dhidi ya Israel katika miezi kadhaa iliyopita.

Baada ya hayo, kituo cha ulinzi wa anga cha Iran kimetangaza katika taarifa yake kwamba: “licha ya maonyo yaliyotolewa na maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu kwa utawala wa kihalifu na haramu wa Kizayuni wa kujiepusha na vitendo vyovyote vya chokochoko, utawala huo bandia umeshambulia baadhi ya vituo vya kijeshi katika mikoa ya Tehran, Khuzestan na Ilam katika hatua ya kuzusha mvutano”. Taarifa hiyo imesema: Hata hivyo, mfumo wa ulinzi wa anga wa nchi umefanikiwa kuzuia na kuzima kitendo hicho cha uchokozi licha ya uharibifu mdogo uliosababishwa na hujuma hiyo.

Israel inajaribu kukuza shambulizi hilo dhaifu na lilifofeli dhidi ya Iran, na wachambuzi wengi wa mambo wanaamini kuwa, mashambulizi ya leo hayawezi kulinganishwa na Operesheni Ahadi ya Kweli-2. Katika opereshini hiyo, Iran ilitumia kwa uchache makombora 180 ya balestiki dhidi ya shabaha za kijeshi na kiusalama za utawala wa Kizayuni, na kwa mujibu wa Washington Post, kwa akali, makombora 20 kati ya hayo yalipiga Kambi ya Anga ya Navatim, na makombora mengine matatu yalitwanga kambi ya “Tel Nouf” katikati mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel pia alikiri kuhusu ukali na ukubwa wa shambulizi la Iran katika Operesheni Ahadi ya Kweli-2 wakati aliposema baada ya shambulio hilo kwamba: “Walirusha mamia ya makombora dhidi yetu katika mojawapo ya mashambulizi makubwa zaidi katika historia.”

Aidha baada ya Operation ‘True Promise 2, mchambuzi wa masuala ya Asia Magharibi, “Jotham Confu” aliandika katika gazeti la Telegraph la Uingereza kwamba: “Iran imethibitisha kuwa ina uwezo wa kupenya mfumo mkubwa zaidi wa ulinzi wa anga.”

Operesheni Ahadi ya Kweli 1 na 2, ambazo zilikuwa jibu kwa uchokozi wa utawala ghasibu wa Israel na ambayo ilifanyika kwa mujibu wa Ibara ya 51 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa na hatua ya kuwajibika na ya kimantiki ya kulinda amani na usalama wa kanda wa Magharibi mwa Asia, ilifichua udhaifu wa mifumo ya ulinzi ya utawala wa Kizayuni ambao ulikuwa ukipigiwa debe na kusifiwa kupita kiasi na vyombo vya propaganda vya Wazayuni na nchi za Magharibi.

Alaa kulli hal, vyombo husika vya Iran vimetangaza kuwa vinatathmini shambulizi hilo la Israel kwa ajili ya hatua inayofuata na vinasisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inahifadhi haki yake ya kujibu aina yoyote ya uchokozi, na hakuna shaka kuwa Israel itapata jibu mwafaka kwa hatua yoyote ambayo imechukua”.