
Dar es Salaam. Ikiwa miezi saba imebakia kuingia kwenye uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Chama cha Mapinduzi (CCM), kimehamasisha wanachama wake wa mkoani hapa kujitokeza kwa wingi kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la mpigakura ili kitetee nafasi ya kushika dola.
Kimesema nguvu walizoanza tangu kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwaka 2024 ambapo walishinda kwa asilimia 98 zinapaswa kwenda kuonekana kwenye uchaguzi wa madiwani, wabunge na urais.
Shughuli ya uboreshaji taarifa za mpigakura zitakazomwenzesha kila Mtanzania kupata kibali cha kutumia haki yake ya kumchagua kiongozi anayemtaka inasimamiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), na kwa Mkoa wa Dar es Salaam linatarajiwa kuanza Machi 17 hadi 23 mwaka huu.
Akihamasisha shughuli hiyo kwenye mkutano wa ndani uliofanyika Wilaya ya Ubungo, ukiwakutanisha viongozi wa chama hicho, jumuiya ngazi ya shina, tawi, mitaa, kata na wilaya, Katibu wa NEC, Itikadi Uenezi na Mafunzo CCM, Amos Makalla amesema ili watete dola ni lazima wafuasi wao wajiandikishe kabla ya kuanza kuwashawishi Watanzania wengine.
“CCM tuna wanachama milioni 12 nchi nzima lakini Dar es Salaam tunaongoza kwa idadi ya wapigakura wengi ikilinganishwa na mikoa mingine, tusilale mtihani tulionao kwanza kuhakikisha idadi hiyo wanajitokeza kujiandikisha viongozi wa wilaya, kata, matawi , mitaa hadi shina hakikisheni watu wenu wanakwenda kujiandikisha, ” amesema Makalla nakuongeza. “Tulifanya kazi kubwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa tunahitaji kukamilisha mpango wetu wa kutetea dola, na kujiandikisha ni mwanzo wa ushindi wetu tusifanye makosa.”
Makalla amesema licha ya kuhitaji kutetea dola lakini uchaguzi ni namba kwani anayepata kura nyingi anatangazwa mshindi hivyo wasipuuze mchakato huo kama wanataka kuitawala nchi.
“Wapiga kura wako ngazi ya chini huku wilayani ni kuratibu tu lakini watu wako kwenye mashina, tawi na kata kwa hiyo watu wa wilayani tokeni simamieni kazi hiyo mkoani na mabalozi na nyie wapeni ushirikiano tusifanye makosa,” amesema.
Makalla ambaye ni mlezi wa chama hicho mkoa wa Dar es Salaam amesema hataki kuona wananchi wakimuangusha katika uboreshaji daftari la kudumu la mpigakura kwani walishafanya makubwa na hapaswi kujikwaa kwa jambo hilo.
“Mkitoka hapa wekeni kwenye ratiba zetu kuanzia Machi 17 hadi 23, 2025 na nyie kama viongozi anzeni na watu wenu wanaowazunguka na baada ya hapo hamasisha wengine ili tujihakikishie kura katika uchaguzi mkuu,” amesema.
Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo amesema wamejipanga kwa uchaguzi mkuu na kumuhakikishia mgeni rasmi huyo CCM itapata ushindi. “Na ushindi unaanzia Machi 17 siku ya kuanza kuboresha daftari la mpigakura, kila mwanaCCM ajitokeze kupiga kura, ili tujihakikishie namba siku ya uchaguzi,” amesema Profesa Mkumbo.