Tanga. Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza atafutwe mwekezaji atakayejenga barabara ya Handeni-Kiberashi-Kijigu hadi Singida kwa mtindo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), kisha watumiaji walipie.
Hatua hiyo amesema inalenga kurahisisha gharama za usafirishaji mizigo kutoka na kuingia Bandari ya Tanga.
Uamuzi wa barabara hiyo kujengwa kwa mtindo wa PPP, amesema unatokana na kutaka ikamilike kwa haraka, jambo alilosema halitawezekana iwapo itaachiwa Wizara ya Ujenzi.
Rais Samia amesema hayo jana alipozungumza na watumishi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), baada ya kuweka jiwe na msingi la uzinduzi wa mradi wa kuboresha Bandari ya Tanga.
Ujenzi wa barabara hiyo ni mwendelezo wa mikakati ya Rais Samia ambaye Februari 28 akiwa mkoani Tanga amesema miongoni mwa matamanio yake ni kuurejesha mkoa huo kuwa wa viwanda, kama ulivyowahi kuwa kabla.
Katika kulifanikisha hilo, amesema tayari Serikali imeanza kuchukua hatua za kupanua viwanda vilivyopo na kujenga vipya ili kutoa fursa za ajira kwa wananchi.

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa katika Bandari ya Tanga mara baada ya kukagua maboresho ya gati mbili mpya wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Tanga Machi 1, 2025.
Mkakati huo amesema utaleta suluhu ya changamoto ya ajira na kupunguza watu wanaokaa vijiweni kunywa kahawa na kupiga umbea.
Akizungumzia barabara itakayojengwa kwa mfumo wa PPP, Rais Samia amesema itagharimu Sh340 bilioni, hivyo itachochea biashara katika Bandari ya Tanga, kwa kuwa ndiyo njia rahisi na yenye gharama nafuu kupitika kwa usafirishaji wa mizigo.
Rais Samia amesema barabara hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya bandari na kwamba, ameshazungumza na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ijengwa kwa mfumo wa PPP akisema wakipitia Wizara ya Ujenzi, barabara hiyo haitakamilika haraka.
Amezitaka wizara hizo mbili zikubaliane na kwa pamoja zitafute mwekezaji atakayeshirikiana na Serikali kuijenga kwa viwango vinavyotakiwa.
“Maana yake hii ndiyo barabara tutakayoitegemea ibebe mizigo mizito kutoka Tanga na kupeleka kwingineko, kwa hiyo ijengwe kwa viwango tunavyovitaka iwekewe mageti watu walipe,” amesema.
Amesema mwekezaji badala ya kulipwa na Serikali inapaswa ajilipe kwa barabara hiyo.
“Sasa kina Azim (Dewji) mje mseme tunalipishwa maana yake pale, tunalipishwa, lazima twende kwa mtindo huo, tuwaweke wenye fedha zao wajenge halafu ninyi mtumie na mlipe,” amesema.
Amesema raia wa kawaida atakayejipitisha ametaka mwenyewe na atalazimika kulipa, lakini lengo la Serikali ni magari ya mizigo ya kibiashara.
“Nalisema mapema kwa sababu tukianza watu wakiona tu mageti siasa zinaanza, huyu mama anatuwekea, tulipe barabara, kayaona wapi, toka uhuru hatujalipa barabara olololo… Watanzania mnajijua si ndiyo,” alisema na kuibua vicheko kutoka kwa wahudhuriaji.
Amesema: “Hakuna Rais kichaa hapa ambaye atafanya jambo la kuwadhuru wananchi wake, hayupo. Ukiona tunaanzisha jambo ujue tumeshapima mara tatu na tuna hakika litaleta faida kwa nchi yetu.”

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri wa Uchukuzi, Prof Makame Mbarawa katika Bandari ya Tanga mara baada ya kukagua maboresho ya gati mbili mpya wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Tanga Machi 1, 2025.
Serikali kupitia PPP ina mpango mwingine wa kujenga barabara ya kulipia kutoka Kibaha hadi Morogoro.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 130 inalenga kupunguza msongamano, Serikali ikikusudia kuunganisha majiji ya Dar es Salaam na Dodoma kwa barabara za express way (barabara ya haraka).
Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ilijenga daraja kuelekea Kigamboni ambalo wananchi wanaolitumia wanalipia.
Kwa mara kadhaa kumekuwa kuiibuka mijadala kutoka kwa wananchi na hata wabunge wakihoji ni kwa nini walipishwe wakati wananchi maeneo mengine ya madaraja hawalipishwi.
Kuhusu bandari
Rais Samia ameeleza kuridhishwa na maboresho ya utendaji.
Amesema miaka ya nyuma hali ilikuwa mbaya zaidi katika utendaji ndani ya TPA.

“Huko nyuma nilikuwa nakaa najiuliza unakuta bodi nzima (ya TPA) inamtetea mtu mhujumu na wanajua hawa wanahujumu, lakini bodi inasimama kuwatetea. Lakini sasa hivi kidogo yale sijayaona,” amesema.
Ameisihi bodi kwa kuwa imekasimiwa madaraka ya usimamizi, iwasimamie vema watendaji wa bandari zote na wajitahidi kuviepuka vitendo vya kuhujumu uchumi.
Amefafanua kuhusu mradi wa uboreshaji wa Bandari ya Tanga, Rais Samia alisema utekelezaji wake utagharimu Sh429.16 bilioni.
Amesema kazi hiyo si tu imeifufua bandari bali imeongeza ufanisi na sasa muda wa kushusha mizigo umepunguza kutoka siku tano hadi mbili.
“Nataka kurudisha hadhi ya Tanga, iwe Tanga ya viwanda Tanga yenye bandari kubwa lakini pia, Tanga ya uvuvi, ndicho ninachokifanya sasa na Mungu atujalie,” amesema.
Amesema kwa sasa Tanga, Dar es Salaam na Bagamoyo ndiyo malango ya Afrika Mashariki kuingia Tanzania na kusambaza mizigo Afrika Mashariki.
Rais Samia amesema mkazo wa Serikali katika uwekezaji unalenga kuongeza upatikanaji wa fedha ili kupunguza utegemezi wa mikopo.

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na wafanyakazi wa Bandari ya Tanga mara baada ya kukagua maboresho ya gati mbili mpya wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Tanga Machi 1, 2025.
Amesema Serikali inatarajia uwekezaji unaofanywa katika bandari, uongeze ufanisi kwani kila kinachofanywa na bandari shindani nazo zinawekeza.
Rais Samia ametaka gharama za upitishaji mizigo katika bandari za Tanzania ziendelee kushushwa ili wafanyabiashara waone sababu ya kuzitumia.
Amesema wafanyakazi wa bandari wanawajibika kujifunza ili kuendana na mahitaji ya ujuzi stahiki kwa dunia ya sasa na kuendana na maboresho.
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema mradi huo ulitekelezwa na mkandarasi M/S China Harbour Engineering Company (CHEC) katika awamu mbili.
Amesema maboresho yameleta mafanikio katika ufanisi wa Bandari ya Tanga.
Ameeleza uwezo wa kuhudumia shehena umeongezeka kutoka tani 750,000 hadi tani milioni tatu kwa mwaka, huku idadi ya meli zilizoingia bandarini ikiongezeka kutoka 118 mwaka 2019/2020 hadi 307 mwaka 2023/2024.
“Muda wa kuhudumia meli umepungua kutoka siku tano hadi siku mbili, jambo lililopunguza gharama za uendeshaji na kuvutia wateja zaidi,” amesema.
Kwa upande wa mapato, amesema yameongezeka kutoka Sh17.23 bilioni mwaka 2019/2020 hadi Sh38.70 bilioni mwaka 2023/2024.
“Kwa miezi saba pekee ya mwaka wa fedha 2024/25, tayari TPA imekusanya Sh49.84 bilioni, haya ni mafanikio makubwa kuwahi kutokea katika bandari hii,” amesema.
Katika hatua nyingine, Rais Samia ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha gesi asilia cha GBP.
Kwa kuwa kampuni hiyo ina hifadhi kubwa ya mafuta, ametaka wasambazaji wasilazimike kwenda kufuata Dar es Salaam badala yake wachukue Tanga.
Amesema kama kuna masuala ya kisera na kisheria yanayohitaji kufanyiwa kazi, ifanyike haraka ili wasambazaji wasilazimike kufuata mafuta Dar es Salaam, wanaacha Tanga ambayo ni jirani kwao.