Mkakati mpya utakavyopunguza vifo vya watoto wachanga

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imezindua fomu mpya ya uandikishaji kwa watoto wachanga wanaolazwa ‘register’ ikiwa ni mkakati wa kupambana na vifo vya watoto wachanga.

Kabla ya uwepo wa register hiyo, taarifa za watoto wachanga zilikuwa zikiandikishwa katika kadi la mama mjamzito au register za wagonjwa wanaolazwa ambao ni watu wazima, hivyo kukosa taarifa za msingi zinazomuhusu mtoto mchanga.

Takwimu zinaonesha mwaka 2019 kulikuwa vifo 24 kati ya vizazi hai 1,000 na takwimu za mwaka 2023 vilipungua kufika vifo 19 kati ya vizazi hai 1,000, hata hivyo hakukuwa na takwimu zinazoonyesha sababu ya vifo hivyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo Jumanne, Machi 4, 2025 Mratibu wa afya ya mtoto na mtoto mchanga kutoka Wizara ya Afya, Dk Angela Leonald amesema licha ya kupungua kwa vifo vya watoto wachanga, wamekuja na mfumo huo ili kubaini visababishi.

“Tulianzisha wodi maalumu za watoto wachanga mpaka sasa tuna wodi 362 zilizo katika hospitali na vituo vya afya, lakini hatukuwa na sehemu ya kuandika taarifa zao.

“Mtu mzima akilazwa kulikuwa na sehemu ya kuandika taarifa zake ni nani, anaumwa nini, amelazwa kwa muda gani na kama amepona ameruhusiwa au amefariki, lakini watoto wachanga hatukuwa na wodi awali na hakukuwa na mfumo wa kujaza taarifa zao,” amesema Dk Angela.

Amesema wizara imegundua kuwa vifo vingi vya watoto wachanga vinaweza kuzuilika, “tumegundua watoto wengi wanalazwa na hatuna sehemu ya kujaza taarifa zao hivyo tumeona kuna umuhimu wa kuwa na register za watoto, watoa huduma wajaze lakini pia itatusaidia kuona viashiria vinavyosababisha vifo vya watoto wachanga.”

Amesema hiyo itasaidia Serikali kuja na mikakati ya kusaidia kupunguza vifo vya watoto wachanga, kwani takwimu zitapangwa kulingana na viashiria vinavyoonekana kutokana na taarifa waliyonayo.

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mary Shadrack amesema wakati wote Serikali imekuwa ikitumia register iliyokuwa na madodoso ya mgonjwa ya rika zote.

“Yaliyomo mule ndani yaliwahusu watu wazima, haikuwa ikionyesha umri wa mtoto mchanga kama ana saa au wiki mbili ilikuwa ngumu kumuhudumia.

“Hii register mpya kuna eneo linasema aina ya ulemavu wa mtoto wakati wa kuzaliwa, na mengine ambayo yatasaidia katika kukusanya takwimu za watoto, itatusaidia utekelezaji wa mikakati na utungaji wa sera kuanza kuwatambua mapema,” amesema.

Mary amesema dodoso hilo litasaidia kuionyesha Serikali iwekeze eneo gani kwani amesema imekuwa vigumu kupunguza vifo vya watoto wachanga kutokana na makisio ya sababu za vifo hivyo.

Kwa mujibu wa daktari bingwa mbobezi wa watoto nchini, Profesa Karim Manji amesema kwa miaka mingi kukosakana kwa register hiyo iliwafanya wataalamu, wanasayansi na Serikali kushindwa kutambua chanzo cha vifo hivyo na kushindwa kupanga mikakati ya kuvipunguza.

“Mwaka 2008 nilipofanya utafiti kuangalia hali halisi ya watoto wachanga nchini, katika mikoa sita tuliona takwimu ni shida sana wakati huo tulikuwa hatuna Mtuha (Mfumo wa Taarifa za Utoaji wa Huduma za Afya) wala chochote.

“Taarifa ziliwekwa kwenye vikaratasi vya kufungia karanga, hatujui ni wangapi wamezaliwa, wamelavu, waliopata matatizo, waliozaliwa kabla ta wakati au njiti hatukujua, hata Serikali ilipata tabu kuweka mikakati ya kutoa huduma katika mikoa hiyo yote,” amesema.

Amesema hata ilipozinduliwa Mtuha taarifa za watoto wachanga ziliingizwa kwenye takwimu za mama, hivyo vitu muhimu kama madodoso ya mtoto alinyonya baada ya saa moja vimeendelea kukosekana, hali iliyosababisha kukosekana kuwekwa nguvu za kifedha na kiuchumi kushughulikia changamoto ya vifo hivyo.

Profesa Manji (66) amesema takwimu hizo zitasaidia kupanga ni watoto wangapi wamepata ulemavu wa kuzaliwa ili Serikali iwapangie mikakati maalumu, waliofariki kwa sababu ya matatizo ya kupumua, oksijeni na changamoto zingine.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI), Dk Honorati Masanja amesema IHI ilishirikiana na Serikali katika kuandaa register hiyo na kwamba mpaka sasa wataalamu wameshafanya mafunzo kwa njia ya mtandao na kwamba vitabu vitawafikia baadaye.

“Malengo endelevu yanatutaka kufikia mwaka 2030 tuwe tumefika nusu ya hivi vifo, 12 au chini ya hapo kwa hiyo tuna miaka mitano ya kufikia malengo, tunaweza kuongeza kasi ni mlima mrefu lakini naamini tunaweza kuupanda,” amesema Dk Masanja.