
Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea kuvionya vituo vya afya kuacha tabia ya kuzuia maiti kwa kisingizio marehemu ameacha deni la gharama za matibabu, wadau wametaka suala hilo lisizungumzwe kisiasa, badala yake zitumike njia sahihi kukabiliana na changamoto hiyo.
Kauli ya Serikali imetolewa wakati ambao kumekuwa na matukio ya maiti kuzuiwa kwenye vituo vya afya licha ya viongozi kadhaa kukemea na kuonya kuhusu vitendo hivyo. Ya hivi karibuni ilitolewa na Waziri wa Afya, Jenista Mhagama.
Aprili 28, 2025 akiwa mkoani Tabora, Jenista alikemea tabia ya watoa huduma kwenye vituo vya afya kuzuia maiti wakitaka kwanza zilipwe fedha za kugharimia matibabu, kitendo alichosema ni kinyume cha mwongozo.
“Kumekuwa na kelele nyingi za upatikanaji wa maiti, vituo vyote vinavyotoa huduma za afya nchini vitambue kuwa maelekezo ya Serikali hayajabadilika. Ninawaagiza tena waganga wafawidhi, rudini muangalie mwongozo acheni kuleta usumbufu kwa wananchi, hatutaendelea kuwafumbia macho watakaokwenda kinyume cha waraka huu wa Serikali.
“Inashangaza unakuta aliyefariki ndiye alikuwa na uwezo wa kujihudumia na kujilipia matibabu waliobaki hawana uwezo, unapozuia maiti yake unataka afufuke ili ajilipie. Tunashangaa kituo cha kutolea huduma za afya kinapozuia mwili,” alisema Jenista.
Walichosema wadau
Wakati waziri akieleza hayo, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema suala hilo litaendelea kuwa mfupa mgumu endapo litaendelewa kufanywa kisiasa.
Amesema: “Serikali isiishie kukemea na kutoa matamko, hospitali zinatumia gharama kumhudumia mgonjwa na huenda asiseme kama hana uwezo akafuata taratibu zote za ustawi wa jamii, ikitokea amefariki ndipo zinakuja taarifa hana uwezo, je hizi gharama anazibeba nani?
“Nia ya Serikali inaweza kuwa njema kabisa, wananchi wasisumbuliwe lakini katika kutekeleza hili, basi iwe tayari kubeba hizo gharama ili isitokee misuguano. Kuwe na fungu maalumu kwenye vituo ambalo litatumika kugharimia matibabu ya wale waliofariki dunia na kushindwa kulipia wakati wanatibiwa,” amesema.
Dk Nkoronko ameshauri Serikali kutengeneza mazingira yatakayowawezesha wananchi wengi kuwa na uwezo wa kumudu gharama za matibabu kwa kukata bima ya afya.
Ushauri huo umeungwa mkono na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St Johns, Shadidu Ndosa ambaye amesisitiza umuhimu wa kila Mtanzania kuwa na bima ya afya ili kuwa na uhakika wa matibabu.
“Suluhisho la hili si matamko ni bima ya afya kwa wote, kila mtu akiwa na bima itakayogharimia matibabu yake hakutakuwa na matukio ya aina hii. Hospitali ni taasisi zinapaswa kujiendesha na zinajiendesha kutokana na wagonjwa kuchangia matibabu. Kama kutakuwa na watu wanatibiwa halafu hawalipii huduma upo uwezekano wa taasisi hizo kushindwa kuendelea kutoa huduma,” amesema.
Daktari wa binadamu, Elizabeth Sanga amesema vitendo vya hospitali kuzuia maiti ni matokoe ya mfumo mbovu wa kugharimia huduma za afya.
Dk Sanga ambaye ni msemaji wa sekta ya afya wa Chama cha ACT-Wazalendo, amesema chanzo cha tatizo ni ukosefu wa fedha za kutosha kwa hospitali za umma unaosabishwa na bajeti finyu katika sekta hiyo.
Ili kukabiliana na hilo, ameshauri kuwapo mabadiliko ya mfumo wa huduma za afya ili watu wajiunge na mfuko wa hifadhi ya jamii wapate huduma za afya kama fao pamoja na mafao mengine yakiwamo ya pensheni.
Amesema pia ahakuna sheria inayoelekeza namna ya kushughulikia madeni ya wagonjwa waliofariki dunia wakipatiwa matibabu ili kutoa nafasi kwa wafiwa kutetea haki zao mahakamani.
Mara kadhaa Serikali imekuwa ikikemea hadharani uzuiaji maiti. Aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alishawahi kupiga marufuku vitendo hivyo.
Kutokana na malalamiko ya wananchi kuzuiwa kuchukua miili ya marehemu, Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza kuandaliwa utaratibu bora wa kulipia matibabu na kuruhusu maiti kuchukuliwa bila usumbufu.
Septemba 2021, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilitoa Waraka namba 1 wenye mwongozo na maelekezo yaliyojikita katika maeneo mawili: Mosi, kulipia gharama za matibabu ili kuzuia malimbikizo ya madeni kwa wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Pili, ni utaratibu wa kuruhusu ndugu kuchukua mwili wa marehemu katika vituo vya kutolea huduma za afya aliyekuwa na deni la matibabu na namna ya kulipia deni baada ya mwili kuchukuliwa.
Mwongozo unaelekeza mgonjwa aliyefia hospitalini, maiti itaanza kulipiwa baada ya kupita saa 24 tangu mwili kupokewa mochwari. Iwapo alikuwa anahudumiwa kwa msamaha wa matibabu, ndugu waruhusiwe kuchukua mwili wa marehemu.
Kwa mujibu wa mwongozo, iwapo marehemu alikuwa anachangia gharama za matibabu na mauti yamemfika akiwa na deni la gharama za matibabu, ndugu aruhusiwe kuchukua mwili baada ya kufanya malipo.
Kuhusu ndugu wasio na uwezo wa kulipa deni mgonjwa anapofariki dunia, mwongozo unataka kuingia makubaliano ya maandishi na kituo cha kutolea huduma ya namna ya kulipa deni na waruhusiwe kuchukua mwili.