Mchakato huu ni mgumu ukizingatia kuwa unahitaji ushirikiano nadra kati ya serikali na waasi wa M23.
Mitihani hiyo ya kitaifa inayofanywa kote katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati na wanafunzi walio na matarajio ya kujiunga na vyuo vikuu, ilianza Jumatatu na itaendelea hadi katikati ya mwezi Juni.
Kuisambaza mitihani hiyo kote nchini humo ni jambo lililohitaji maafisa wa elimu binafsi kusimamia mchakato wa usafirishaji vifaa vya mitihani kutoka Mji Mkuu Kinshasa na kuvipeleka katika miji inayoshikiliwa na waasi wa M23.
Kuondolewa kwa ada ya mitihani
Jean-Marie Mwayesi Mileka, ni mkaguzi mkuu wa elimu ya kitaifa huko nchini Kongo.
“Tulikuwa miongoni mwa wale waliokwenda kuvichukua vifaa hivyo Kinshasa. Tulipovipokea, tuliwaita washirika wetu wa kiufundi na kifedha kutoka kwenye wizara ya elimu. Tunawashukuru wao kwasababu walisaidia vifaa vikasafirishwa kutoka Kinshasa hadi Beni na kisha Goma halafu hatimaye hapa. Kwa ushirikiano wa timu yetu na washirika, vituo vyote 111 tunavyovisimamia vimehudumiwa. Naweza kukuhakikishia kuwa mitihani ipo katika vituo vyote,” alisema Mwayesi.
Serikali ya Rais Felix Tshisekedi mwezi uliopita ilitangaza inaondoaada ya mitihani kwa wanafunzi wa mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini kutokana na ukosefu wa usalama katika maeneo hayo. Ada hiyo ya mitihani kawaida huwa zaidi ya dola 40 kwa kila mwanafunzi.
Ingawa waasi wa M23 wakiwa walisema awali kwamba wanataka kuiondoa serikali ya Rais Tshisekedi, kiongozi wa waasi hao Bertrand Bisimwa ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa bado wanaitambua Kinshasa kama msimamizi wa mitihani ya kitaifa.
Wanafunzi wajitokeza kwa wingi
Makundi ya haki za binadamu mara kwa mara yamewatuhumu waasi wa M23 kwa kuwauwa raia wakiwemo watoto, madai ambayo kundi hilo limeyakanusha.
Mangala Lubunga ni miongoni mwa wanafunzi waliokalia mtihani huo katika shule moja huko Bukavu.
“Nina furaha, najihisi huru. Wakati wa vita, marafiki zetu walifariki, wengine walikimbilia nchi jirani ila leo, niliweza kumaliza mtihani katika mazingira salama,” alisema Lubunga.
Kulingana na afisa wa elimu Mwayesi, wanafunzi 44,000 waliojisajili kwa mitihani katika eneo lake, karibu 42,000 walijitokeza kufanya mitihani akisema kuwa huenda waliosalia walikimbia kutokana na mapigano.
Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda waliiteka miji miwili mikuu ya mashariki mwa Kongo mapema mwezi huu na kwa sasa wanajaribu kuonyesha kwamba wanaweza kuongoza.
Wakati huo huo viongozi wa Afrika pamoja na Marekani na Qatar, wanajaribu kutafuta makubaliano yatakayofikisha mwisho mapigano hayo.