Mitandao kinara ya kijamii 2025, fursa zake kiuchumi

Dar es Salaam. Katika ulimwengu wa kidijitali, mitandao ya kijamii imekuwa sehemu muhimu ya maisha ya walio wengi, ikiunganisha mabilioni ya watumiaji duniani kote.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, idadi ya watu duniani imefikia takriban bilioni 8.2 huku watumiaji wa mtandao wakiwa bilioni 5.56, wanaotumia simu za mkononi wakiwa bilioni 5.78, na wale wanaotumia mitandao ya kijamii wakiwa bilioni 5.24.

Hii ina maana kwamba asilimia 64.7 ya watu duniani wanatumia mitandao ya kijamii, na asilimia 94.2 ya watumiaji wa mtandao wanatumia angalau jukwaa moja la kijamii kila mwezi.

Mitandao inayoongoza kwa idadi ya watumiaji ni YouTube, Facebook, Instagram, WhatsApp, na TikTok, ambayo kila moja inatoa fursa mbalimbali za kiuchumi na ajira kwa watumiaji.

YouTube inaongoza kwa watumiaji bilioni 3.9 wanaotumia kila mwezi, ikiwa ni jukwaa la video linalovutia wengi.

Inatoa fursa za kupata pesa kupitia mpango wa Programu za Ushirika (YouTube Partner Program), ambapo watengenezaji wa maudhui wanaweza kupata mapato kutokana na matangazo ikiwa wana wafuasi zaidi ya 1,000 na saa 4,000 za kutazamwa kwa mwaka.

Walio wengi wamepata mafanikio kwa kutengeneza maudhui ya kielimu, burudani, au maisha ya kila siku na kuyafikisha kwa watazamaji wa kimataifa.

Facebook, ikiwa na watumiaji bilioni 3.07, inabakia kuwa jukwaa kubwa la kijamii. Hapa, watu binafsi na wafanyabiashara wanaweza kupata pesa kupitia matangazo, uuzaji wa bidhaa kwenye soko lake lijulikanalo kama Marketplace, au kuunda vikundi vya kuuza huduma.

Biashara ndogo zinaweza kutumia matangazo ya Facebook, ambayo yanafikia wateja bilioni 2.2 kila mwezi, ili kukuza mauzo yao. Walio wengi wameanzisha kurasa za biashara za ndani, kama vile za kuuza nguo au chakula, na kupata wateja kupitia majukwaa hayo.

Instagram, yenye watumiaji zaidi ya bilioni 2, inayolenga picha na video fupi, imevutia vijana, kampuni na taasisi mbalimbali. Watumiaji wanaweza kupata pesa kupitia ushirikiano, uuzaji wa bidhaa binafsi, au uuzaji wa washawishi (influencer marketing).

Kwa mfano, mtu mwenye wafuasi wengi anaweza kulipwa na kampuni za urembo au mitindo ili kukuza bidhaa zao.

Zaidi ya asilimia 60 ya watumiaji wa Instagram hufanya ununuzi kupitia jukwaa hilo, hivyo kufanya iwe rahisi kwa wafanyabiashara wadogo kuuza moja kwa moja jukwaani.

WhatsApp, pia ina watumiaji zaidi ya bilioni 2, ni maarufu kwa mawasiliano ya moja kwa moja. Biashara ndogo, kama vile wauzaji wa chakula au utoaji wa huduma, hutumia WhatsApp Business kuwasiliana na wateja, kupokea maagizo, na kutoa huduma za haraka.

Jukwaa hili linawezesha uuzaji binafsi, ambapo mtu anaweza kuunda orodha ya wateja na kuwauzia bidhaa au huduma mara kwa mara.

TikTok, yenye watumiaji zaidi ya bilioni 1.69, inaendelea kukua kwa kasi, hasa miongoni mwa vijana. Jukwaa hili linawapa watumiaji fursa ya kupata pesa kupitia TikTok Creator Fund, ambapo watumiaji wanalipwa kwa maudhui yanayovutia watazamaji wengi.

Aidha, kampuni nyingi hushirikiana na watengenezaji wa maudhui kwenye TikTok ili kukuza bidhaa zao, hasa kwa sababu asilimia 77 ya watumiaji wa Gen Z hutumia jukwaa hili kutafuta bidhaa mpya. Maudhui ya kucheza (dance), elimu, au vichekesho yanayovuma yanaweza kutoa mapato ya mara kwa mara.

Mitandao hii ya kijamii inatoa fursa nyingi za kiuchumi, lakini mafanikio yanahitaji zaidi mkakati, ubunifu, na uvumilivu. Watumiaji wanapaswa kujifunza jinsi ya kutengeneza maudhui yanayovutia, kuelewa watazamaji wao, na kutumia zana za uchambuzi za kila jukwaa ili kuboresha utendaji wao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *