Miss Tanzania 2018 hana mpango na sanaa!

Miss Tanzania mwaka 2018, Queen Elizabeth Makune amesema hana mpango wa kuingia katika muziki, filamu au mitindo kama walivyofanya baadhi ya warembo waliowahi kutwaa taji hilo miaka ya nyuma.

Utakumbuka Queen akitokea kanda ya Dar es Salaam alitwaa taji la Miss Tanzania akiwa na umri wa miaka miaka 22 na kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Miss World 2018 yaliyofanyika nchini China.

Hata hivyo, kabla ya hapo mrembo huyo tayari alikuwa ameshinda taji la Miss World University Afrika 2017 liloshirikisha mataifa 53 ya Afrika nchini Korea hapo Desemba 2017.

“Hapana kwa kweli sijioni upande huo kwa sasa na hata hapo baadaye, kwangu ni mwendo wa biashara na kilimo tu,” Queen ambaye ni msomi wa Shahada ya Uzamili upande wa Uongozi wa Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ameliambia gazeti hili.

Ikumbukwe baadhi ya warembo kutoka Miss Tanzania walioamua kuingia upande wa sanaa ni pamoja na Jacqueline Ntuyabaliwe Mengi  ‘K-Lynn’ (2000) akifanya muziki na Millen Magese (2001) akifanya mitindo na filamu.

Pia kuna Wema Sepetu (2006), akifanya filamu, Genevieve Emmanuel (2010) akifanya muziki na Salha Israel (2011) akifanya filamu.

Wema ndiye Miss Tanzania aliyefanikiwa zaidi upande wa filamu akiwa ameshinda tuzo mbili za Sinema Zetu International Film Festival Award (SZIFF) na tuzo ya Hollywood And African Prestigious Awards (HAPAWARDS) nchini Marekani.

Katika hatua nyingine, licha ya Queen kuweka alama kubwa katika maisha yake kupitia Miss Tanzania ambayo haitafutika, ni vigumu kwake kusahau mafunzo aliyoyapata kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

“JKT nilichaguliwa msichana pekee kwenye darasa langu la PCM kwenda JKT mwaka 2016, nikapiga moyo konde nikaenda, ilikuwa ngumu kweli maana umetoka zako nyumbani unakwenda kule mara mbio za asubuhi, mchana na jioni, sio mchezo,”  anasema Queen.

“Niliwahi kupewa adhabu ya kujaza maji kwenye ndoo kwa kutumia kisoda, jiulize inajaa saa ngapi?, kikawaida kufanya makosa inatokea; kipindi tumeruhusiwa kurudi nyumbani kuja kufanya maombi nikachanganya mafaili, niliporudi ndio nikakutana na hiyo adhabu,”  anasema Queen.

Queen ambaye JKT alipewa jina la ndege kutokana na urefu wake, anaongeza kuwa hilo limemfunza kuwa mvumilivu, mwenye ushirikiano na nidhamu, kubwa yote ndio yanamkamilisha kuwa Queen anayeonekana leo hii.

Ikumbukwe mashindano ya Miss Tanzania kwa mara ya kwanza yalifanyika mwaka 1967 na mrembo wa kwanza kutwaa taji hilo alikuwa ni Theresa Shayo, kisha yalisitishwa hadi mwaka 1994 na mrembo Aina Maeda kunyakuwa taji hilo