Misri Pamoto… Walioshika mechi watajwa

UKIANGALIA kikosi cha Simba kisha ukichungulia pale Al Masry, kuna kitu utagundua kuhusu mastaa wawili, Jean Charles Ahoua na Fakhreddine Ben Youssef ambao Jumatano watakuwa na shughuli nzito ya dakika tisini wakionekana kuishika mechi.

Mastaa hao katika timu zao wanaonekana kuwa ndiyo wamebeba matumaini makubwa ya kufanya vizuri na kuvuka kwenda nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Ipo hivi; Jumatano hii Al Masry itaikaribisha Simba katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya robo fainali utakaochezwa kwenye Uwanja wa New Suez nchini Misri ukiwa ni wa mkondo wa kwanza kabla ya kurudiana Aprili 9 jijini Dar es Salaam.

Takwimu zinaonyesha, Simba wakati inapambana hatua ya makundi na kumaliza kinara wa Kundi A, ilifunga mabao manane huku nyota aliyechangia mengi zaidi ni kiungo mshambuliaji, Jean Charles Ahoua aliyehusika na manne, baada ya kufunga mawili na kuasisti mawili.

Kwa upande wa Al Masry waliomaliza nafasi ya pili Kundi D, Fakhreddine Ben Youssef aliyefunga mabao matatu ya timu hiyo hatua ya makundi kati ya saba, akionekana mshambuliaji huyo raia wa Tunisia ndiye tishio.

Mabao hayo ya Ben Youssef ni sawa na yaliyofungwa na Kibu Denis wa Simba katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, wakizidiwa na Ifeanyi Ihemekwele wa Enyimba FC mwenye manne na kinara, Ismail Belkacemi wa USM Alger aliyefunga matano.

Nyota wengine waliofunga mabao ya Al Masry katika hayo saba iliyoyafunga ni Mahmoud Ramadan aliyefunga mawili, huku Mido Gaber na Mohamed Hashem, wakifunga bao moja kila mmoja wao.

Kwa upande wa Simba, mbali na Kibu Denis mwenye matatu, wengine ni Leonel Ateba na Jean Charles Ahoua ambao kila mmoja amefunga mawili, huku Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ akifunga moja na kuifanya timu hiyo kufunga mabao manane.

Ukimuweka kando Ahoua katika nyota wa Simba waliochangia mabao mengi zaidi, mwingine ni Leonel Ateba akichangia matatu, akifunga mawili na kuasisti moja.

Kwa upande wa Al Masry, nyota wa timu hiyo hawana namba nzuri za kutengeneza mabao kwa sababu, Karim Bambo, Khaled El Ghandour, Salah Mohsen wametengeneza moja kila mmoja wao, wakimtegemea zaidi mshambuliaji, Fakhreddine Ben Youssef.

Kwa nyota waliotengeneza nafasi kubwa, Jean Charles Ahoua wa Simba amewapiga bao tena Waarabu kwani ametengeneza nne, akizidiwa moja tu na beki wa kulia, Fidel De Sousa anayeichezea Black Bulls FC ya Msumbiji anayeongoza akiwa nazo tano.

Kwa upande wa Al Masry inamtegemea kiungo, Khaled El Ghandour ambaye hadi hatua za makundi zinatamatika ametengeneza nafasi kubwa mbili tu, ikionyesha wazi nyota wa Simba wana namba nzuri tofauti na wapinzani wao tangu michuano imeanza.

Pia Ahoua amewapiga bao mastaa wa Al Masry kwa kutengeneza nafasi nyingi kiujumla, kwani ametengeneza 16, sawa na kiungo mshambuliaji, Yassine Labhiri wa RS Berkane ya Morocco, wakizidiwa na Kalu Nweke wa Enyimba FC ya Nigeria aliyetengeneza 18.

Nyota wanaoongoza kwa kupiga pasi sahihi kwa dakika 90, Simba pia inaongoza kwani kiungo wake, Yusuph Kagoma anashika nafasi ya nane, akiwa na usahihi wa 57.1%, nyuma ya beki wa kati, Adam Alilet wa USM Alger ya Algeria anayeongoza na 82.8%.

Alilet anafuatiwa na kiungo mwenzake wa USM Alger, Oussama Chita anayeshika nafasi ya pili akiwa na usahihi kwa 70.7%, huku kwa upande wa Al Masry, Mohamed Sayed Makhlouf anashika nafasi ya 47, baada ya kupiga pasi zenye usahihi kwa 41.4%.

Hata hivyo, licha ya rekodi hiyo nzuri, tangu mwaka 2018, Simba haijawahi kuvuka robo fainali kwenda hatua ya nusu fainali kwa sababu kwa misimu yote mitano kati ya saba ilijikuta ikiishia robo fainali, huku ikidhamiria kuuvunja mwiko huo kwa msimu huu tena.

Kocha wa Simba, Fadlu Davids alisema ameridhishwa kwa kiasi kikubwa na maandalizi ya timu hiyo tangu ilipowasili Misri, huku wachezaji wakionyesha utayari kwa ajili ya mchezo huo mgumu ugenini, jambo linalompa matumaini ya kufanya vizuri.

“Tumekuwa na siku nzuri tangu tumewasili hapa Misri, ni mchezo mgumu ila tumejipanga kucheza kwa tahadhari na kwa kuwaheshimu,” alisema.

Simba iliyomaliza kinara wa kundi A na pointi 13, imepangiwa na Al Masry iliyomaliza ikiwa nafasi ya pili kundi D na pointi tisa, nyuma ya wapinzani wao kutoka Misri, Zamalek ambao ndio mabingwa watetezi wa michuano hiyo msimu wa 2023-2024.

Kitendo cha Al Masry kumaliza nafasi ya pili huku Simba ikimaliza ya kwanza, kimezifanya timu hizo kukutana tena ambapo pambano hilo la Aprili 2, litakuwa ni la tatu kwao kukutana kwa miaka ya hivi karibuni baada ya mwaka 2018.

Timu hizo zilikutana raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo mechi ya jijini Dar es Salaam zilitoka sare ya mabao 2-2, Machi 7, 2018, kisha marudiano Misri zikatoka suluhu (0-0), Machi 17, 2018, na Simba kutolewa kwa mabao ya ugenini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *