Misri na Uhispania zatoa wito mpya wa kusitishwa mapigano Gaza na Lebanon

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Misri na Uhispania walitoa wito huo jana Jumatano wakitaka kusitishwa mapigano mara moja huko Ukanda wa Gaza na Lebanon.

Badr Abdelatty, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amekuwa mwenyeji wa mwenzake Uhispania mjini Cairo.

Abdelatty amesema alipokuwa akizungumza na waandishi habari: “Kiburi cha madaraka hakiwezi kuleta usalama wala amani kwa nchi yoyote, na tuna mafunzo mengi katika siku za nyuma katika eneo hili. Hivyo tunaweza kuamini kuwa mamlaka yoyote tunayofikia hayawezi kutudhaminia usalama na amani isipokuwa kwa kuzingatia haki halali ya watu wa Palestina. Hakuna usalama wala  utulivu unaoweza kupatikana katika eneo hili bila ya kuanzishwa kwa taifa huru la Palestina.”

Naye José Manuel Albares Bueno mwanadiplomasia mkuu wa Uhispania amesema: “Tunataka usitishaji vita wa kudumu na wa mara moja huko Ukanda wa Gaza na mapatano nchini Lebanon.”

Ameendelea kusema: “Hili ndilo ombi ambalo Uhispania na Misri pamoja na washirika wengine wengi katika jamii ya kimataifa wamekuwa wakilitoa tangu kuanza ghasia na vita vya hivi sasa, kwanza kabisa, huko Gaza na kisha Lebanon. Tunazungumzia hapa juu ya nchi huru inayojitawala.”

Uhispania ni moja ya nchi tatu za Ulaya ambazo ziliitambua Palestina kama taifa huru mnamo Mei.

Wiki iliyopita Waziri Mkuu wa Uhispania aliitaka EU kukubali ombi la kusimamisha biashara na utawala dhalimu wa  Israel.

Pedro Sanchez pia, ametoa wito kwa watengenezaji wa silaha kuacha kuuzia utawala huo silaha.