Mishahara iendane na kazi, hali ya maisha

Takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuhusu ajira na mapato katika sekta rasmi kwa mwaka 2022/23 zimeonyesha hali inayotia wasiwasi kuhusu viwango vya mishahara nchini.

Kulingana na ripoti hiyo, mtu mmoja kati ya wawili walio katika sekta rasmi analipwa mishahara isiyokidhi mahitaji. Hii inadhihirisha changamoto kubwa kwa wafanyakazi wengi, hasa wale walioko katika sekta binafsi ambako mishahara midogo imetawala.

Sekta binafsi, licha ya kuajiri idadi kubwa ya watu, imetajwa kuongoza kwa kutoa mishahara ya kiwango cha chini. Ripoti inaonyesha kuwa zaidi ya watu milioni 1.9 kati ya takribani milioni 3.7 walio katika ajira rasmi, wanalipwa chini ya Sh500,000.

Kwa upande mwingine, sekta ya umma inaonyesha tofauti kubwa, kwani hakuna mfanyakazi anayelipwa chini ya Sh300,000.

Gharama za maisha zinaendelea kupanda kila uchwao kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu kama chakula, nishati, usafiri na kodi za makazi, achilia mbali huduma kama za elimu na matibabu.

Kwa mfano, bei ya sukari ambayo ilikuwa Sh1,700 kwa kilo miaka 10 iliyopita, sasa inafikia kati ya Sh3,000 na Sh3,500. Hii inamaanisha kuwa mfanyakazi anayelipwa chini ya Sh500,000 kwa mwezi ana mzigo mkubwa wa kifedha, ambao hawezi kuubeba bila kuathiri ustawi wake wa maisha.

Tunatambua kuwa zipo sababu za waajiri hao ambao kwa namna moja au nyingine wamebeba mzigo mkubwa wa kuajiri watu wengi katikati ya changamoto za kiuzalishaji, lakini tunawiwa kusisitiza kuwa mishahara inayolipwa iendane na gharama za maisha.

Mishahara midogo inaleta athari si tu kwa wafanyakazi, bali pia kwa uchumi mzima. Wafanyakazi wanaolipwa chini ya kiwango kinachowezesha maisha ya heshima wanakosa motisha kazini, jambo ambalo linaathiri pia uzalishaji na ubora wa kazi wanayoifanya. Aidha, mshahara mdogo unawasukuma baadhi ya wafanyakazi kujiingiza katika shughuli zisizo za kimaadili kama njia ya kujiongezea kipato. Hii ni hatari kwa maendeleo ya taifa.

Ni muhimu kwa Serikali, waajiri na vyama vya wafanyakazi kushirikiana kuhakikisha kuwa mishahara inalipwa kwa kuzingatia hali halisi ya maisha na mchango wa mfanyakazi kazini.

Wakati sekta ya umma imeanza kurejesha nyongeza ya mishahara kila mwaka, sekta binafsi nayo inapaswa kufuata mkondo huo kwa kuhakikisha kuwa mishahara inakua kwa uwiano na kupanda kwa gharama za maisha na kulingana na ushawishi wa taasisi wanazozifanyia kazi.

Serikali kupitia Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) inapaswa kufanya utafiti wa kina kuhusu uwiano wa mishahara na gharama halisi za maisha, ili kubaini mianya inayosababisha wafanyakazi wengi kuendelea kupata malipo duni.

Aidha, hatua madhubuti zinapaswa kuchukuliwa kuhakikisha waajiri wote wanazingatia kima cha chini cha mshahara kilichowekwa na Serikali ili kuepusha unyonyaji wa wafanyakazi.

Katika taifa linalolenga kukuza uchumi wake na kuboresha ustawi wa wananchi wake, mishahara inapaswa kuendana na hali halisi ya maisha. Kwa kufanya hivyo, si tu kwamba wafanyakazi wataweza kuendesha maisha yao kwa heshima, bali pia uchumi utaimarika kupitia ongezeko la matumizi, uzalishaji na kodi zitokanazo na mishahara zitachangia pakubwa katika uchumi.

Ni wakati sasa kwa vyombo husika kuchukua hatua kuhakikisha wafanyakazi wote wanalipwa mishahara inayowawezesha kuishi maisha yenye staha.