
Unguja. Katika kubuni vyanzo vipya vya kutekeleza miradi ya maendeleo kisiwani Zanzibar, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imeanzisha Hati Fungani (Sukuk) inayofuata misingi ya sharia ambayo itatumia fedha hizo zinazowekezwa na wanachi na wadau wengine kutekeleza miradi hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya amesema uanzishaji wa hati fungani hiyo utaiwezesha Serikali kuwa na uwanja mpana wa kupata fedha kwa ajili ya miradi badala ya kutegemea mikopo na vyanzo vingine.
Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Februari 13, 2025 wakati wa Uzinduzi wa Bodi ya Hati Fungani (Sukuk) na kukabidhi nyaraka muhimu kwa bodi hiyo. Sukuk ni chombo kilichopo chini ya hazina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Kwa hiyo tukio hili la leo linatuelekeza kutufikisha kule tunapotakiwa kufika, fedha zinazopatikana zinawekezwa katika miradi ambayo haikinzani na sharia na uwekaji wa hesabu na mchakato mzima unaendana kwa muktadha wa shariah,” amesema Dk Saada.
Ametaja miongoni mwa faida za kuwekeza katika hati fungani hiyo inayofuata misingi ya sharia na kumilikiwa na SMZ kwa asilimia 99, ni uwazi kwani mtu anayewekeza anafahamu fedha zake alizowekeza zinakwenda kufanya jambo gani.
“Yule anayewekeza jambo linatangazwa kwa umma tofauti na hatifungani nyingine, hazitangazwi, pia inatoa faida badala ya riba kulingana na uwekezaji uliofanywa na mtu, huku mwekezaji mwenyewe anakuwa hana wasiwasi kwani anapata umiliki,” amesema.
Faida nyingine itakayopatikana katika hatifungani hiyo inayodumu kwa miaka saba, kila baada ya miezi sita mwekezaji anapata faida ya asilimia 10.5
Kwahiyo itamfanya mtu kuona kwamba fedha zake zimewekezwa kwenye Sukuk na miradi inatekelezwa faida yake anapata kuazia miezi sita hadi miaka saba,” amesema.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), Arafat Ali Haji amesema kupitia huduma za PBZ IKHALAS wamechaguliwa kuwa benki ambayo itapokea fedha ambazo wananchi na wawekezaji mbalimbali watawekeza katika hati fungani hiyo ya serikali.
Pia ndio itakuwa benki mlipaji wa zile gawio ambayo yatakuwa yanalipwa kila bada ya miezi sita kutoka kwa mwekezaji.
“Kwahiyo majukumu yetu ni hayo mawili kwanza kupokea zile fedha zote kutoka Tanzania ama wawekezaji wote watakaotaka kuwekeza kuingiza katika miradi watakuwa wakizitumia kutokea benki ya PBZ,” amesema Arafat.
Mwenyekiti Mtendaji Yusra Sukuk Co Ltd ambao ndio washauri elekezi, Sheikh Mohamed Issa amesema fedha zitatolewa anapewa serikali kujenga miradi ya maendeleo na miradi hiyo wanatamani iandikwe majina ya Sukuk.
Amesema kampuni hiyo hisa zake zinamilikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa asilimia 99 na hisa moja inamilikiwa na mmoja wa watendaji wa serikali kwa mujibu wa sheria za nchi.
“Sukuk ya Zanzibar imekidhi misingi ya shariah, kwahiyo inakabidhiwa na cheti kwa misingi ya shariah,” amesema.
Amesema kwa mujibu wa sheria za kimataifa lazima kuwe na mwenye dhamana ya kutangaza kuna katika hati hiyo atakayetaka fedha kwa ajili ya maendeleo ni serikali.
Amesema kwa mujibu wa sheria za masoko ya mitaji na dhamana, lazima kuwe na watu wanaosimamai na kutoa maoni na kutayarisha nyaraka zitakazoplekwa kwa wawekezaji ambao ni mshauri kiongozi, washauri wa mambo ya shariah wakiwa chini ya kituo cha usimamizi za kifedha za kiislam na mshauri wa mambo ya sheria.
Amesema Sukuk itawekezwa kidigitali hata mtu akiwa nyumbani anaweza kuwekeza kupitia simu yake.
Mwenyekiti wa Zanzibar Treasury Sukuk one Ltd (SPV), Juma Amour Mohammed amesema Sukuk ni muhimu katika nchi na ni muhimu kwa wananchi na taasisi zitapata sehemu muhimu ya kuwekeza fedha zake.
“Hili ni muhimu kwa nchi kwani itaweza kufanya miradi mbalimbali itakayotokana na Sukuk hii, kwahiyo tunatakiwa sote kuwa pamoja..” amesema.