
Katika mkutano wa Bunge unaoendelea jijini Dodoma, mjadala kuhusu mipango ya maendeleo ya kitaifa umechukua nafasi yake.
Wabunge wamekosoa na kushauri kuhusu umuhimu wa miradi ya maendeleo kuwa na athari za moja kwa moja kwenye maisha ya wananchi kwa kuondoa umasikini.
Ni dhahiri kuwa Tanzania, kwa miongo mingi, imekuwa na mipango mizuri na miradi mingi yenye nia ya kuimarisha uchumi na kuinua hali ya maisha ya watu, lakini matokeo hayajafikia viwango vinavyotarajiwa.
Kwa kuwa hali ya umasikini bado ni changamoto, miradi ya maendeleo inapaswa kulenga moja kwa moja kuondoa hali hiyo na kuhakikisha kuwa rasilimali zinazowekezwa zinatoa matokeo yanayoonekana kwa mwananchi wa kawaida.
Katika mjadala huo, ulitolewa wito wa kuwekeza zaidi kwenye sekta ya kilimo, ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania. Sekta hii ni msingi muhimu wa uchumi wa Taifa, lakini inakosa tija inayotarajiwa, licha ya uwekezaji mkubwa unaofanyika kila mwaka.
Changamoto kubwa ni kuwa miradi mingi inayotekelezwa, kama vile “Jenga Kesho iliyo Bora” na ujenzi wa mabwawa ya kilimo cha umwagiliaji, haijaweza kuleta matokeo ya kuridhisha. Hii inaonyesha hitaji la tathmini ya kina ya kila mradi ili kubaini ni kwa kiasi gani unachangia kuondoa umasikini wa wananchi.
Mbali na miradi hiyo ya kilimo, upo umuhimu wa kufanyia tathmini miradi mikubwa ya miundombinu kama Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere na SGR ili kujua kwa undani faida itakayopatikana. Miradi mikubwa kama hii inatumia kiasi kikubwa cha fedha za walipa kodi, na hivyo ni muhimu fedha hizi zitumike kwa ufanisi mkubwa, kuhakikisha kuwa zinaimarisha uchumi kwa kuwahusisha wananchi moja kwa moja kwenye shughuli za uzalishaji. Kupitia tathmini hizi, Serikali itapata fursa ya kuzingatia maeneo ambayo bado yana changamoto na kuweka mikakati itakayosaidia kuboresha matokeo.
Sekta ya viwanda imekuwa pia ikitajwa mara nyingi kama njia muhimu ya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na kuongeza ajira. Serikali ilianzisha sera ya kujenga viwanda, hususan viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo, kama njia ya kuongeza thamani ya mazao na kukuza uchumi wa ndani.
Pia, wabunge walijadili kuhusu matumizi ya rasilimali za kitaifa katika miradi inayofanana kwenye taasisi mbalimbali, kama vile ununuzi wa vifaa vya kuchimba mabwawa na kutengeneza barabara. Matumizi haya yamekuwa mzigo kwa Serikali, huku baadhi ya vifaa vikitumika muda mfupi na kwa gharama kubwa.
Wabunge walipendekeza kuwa vifaa hivi vingeweza kuwekwa sehemu moja na kuvikodi kwa taasisi mbalimbali zinazovihitaji, hivyo kupunguza gharama kwa Serikali na kuongeza ufanisi.
Kuhusu elimu, Serikali inahitaji kuwa na mipango bora ya kuimarisha ubora wa vyuo vikuu kwa kuweka msisitizo kwenye umahiri na ubobezi wa masomo. Mfano, badala ya kujenga miundombinu mipya, ni bora fedha hizi zingeelekezwa kuboresha miundombinu na uwezo wa ile iliyopo ili kufikia malengo hayo.
Kwa kuzingatia hoja zilizotolewa, ni wazi kuwa Tanzania inahitaji kubadilika kutoka kuwa Taifa la mipango na mikakati isiyoleta matokeo, na badala yake kuwa taifa linalofanya tathmini za kina na kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa kila mradi ili kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo inaleta tija kwa wananchi, ikichochea ukuaji wa uchumi na kuondoa umasikini.