Minziro atoa kauli nzito dhidi ya Namungo

KOCHA Mkuu wa Pamba Jiji, Fredy Felix ‘Minziro’ amesema ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Mashujaa FC kwenye Kombe la Shirikisho (FA) na kutinga robo fainali umekipa kikosi chake motisha na hali ya kujiamini ambayo itawasaidia kesho kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo.

Pamba Jiji FC itakuwa mwenyeji wa Namungo FC katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kuikaribisha katika mchezo wa Ligi Kuu namba 186 wa raundi ya 24 utakaochezwa kuanzia saa 8:00 mchana.

Wenyeji hao, wanakamata nafasi ya 13 baada ya michezo 23 wakivuna alama 22, wakiwa wameshinda mechi tano, sare saba na kupoteza 11 huku wakifunga mabao 14 na kuruhusu 25.

Wakati huo Namungo yenye alama 23 inakamata nafasi ya 12 baada ya kushinda michezo sita, sare tano na kupoteza 12, huku ikifunga mabao 16 na kuruhusu 28.

Minziro amesema licha ya kwamba utakuwa mchezo mgumu kutokana na uwiano wa alama kati yao, lakini ni mechi muhimu kwa kikosi chake kuhakikisha kinapata alama tatu na kutimiza malengo ya klabu ya kutoshuka daraja.

“Tumerudi kwenye ligi ambayo kila mmoja anapigana kuhakikisha anapata ushindi
Matokeo mazuri dhidi ya Mashujaa kwenye FA (Kombe la Shirikisho) yametuongezea kujiamini vijana wameongeza morali,” amesema Minziro na kuongeza:

“Tunakutana na timu nzuri wana kocha mzuri na sisi tumejiandaa vizuri kukabiliana nao, kwa ujumla timu yetu iko vizuri tumejipanga kukabiliana na hilo ili tupate alama tatu.”

Kiungo wa Pamba Jiji, Michael Samamba amesema ligi imekuwa ngumu kutokana na makocha wengi kufahamiana mbinu, ubora na kuwa na uzoefu na kila moja kupambana isishuke daraja jambo ambalo wanalitegemea katika mchezo wa kesho dhidi ya Namungo.

“Tumejipanga wachezaji kuhakikisha tunabakiza alama tatu nyumbani ili kuipambania timu yetu, mashabiki wetu, sisi wachezaji na malengo ya klabu. Muhimu ni alama tatu tunapambana kadri tutakavyoweza kuhakikisha mwisho wa msimu hesabu zetu zinakwenda vizuri na tunakuwa na furaha,” amesema Samamba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *