
KOCHA wa Pamba Jiji, Fred Felix ‘Minziro’, amejikuta kwenye presha kubwa kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo katika mechi mbili zilizopita za ligi, hali inayochochea madai baadhi ya wachezaji wake hasa wa kigeni wanashindwa kuelewa mbinu zake za kiufundi.
Minziro ambaye alichukua nafasi ya Goran Kopunovic Oktoba 2024, amepewa muda mfupi kubadili mambo katika kikosi hicho, huku uongozi wa timu hiyo ukitaka kuona mabadiliko ya haraka ili kuepusha hatari ya kushuka daraja.
Presha dhidi ya kocha huyo imeongezeka zaidi baada ya kupoteza michezo miwili mfululizo, dhidi ya Yanga kwa mabao 3-0, na Kagera Sugar 2-1. Matokeo haya yameifanya Pamba Jiji kushika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi, ikiwa na alama 22 ikicheza mechi 23, hali inayowafanya kuwa miongoni mwa timu zinazokabiliwa na hatari ya kushuka daraja zikisalia mechi saba.
Taarifa kutoka katika klabu hiyo zinadai kuna mgawanyiko katika kikosi hicho na baadhi ya wachezaji wa kigeni hawajakubaliana na mbinu za Minziro, jambo linalohusishwa na matokeo mabaya.
Chanzo cha kuaminika kimeliambia Mwanaspoti: “Tatizo kubwa ni kuna wachezaji wa kigeni ambao hawajazoea mbinu za kocha. Uongozi umempa muda wa kurekebisha hali hii, lakini presha ni kubwa kwa sababu hatutaki kushuka daraja.”
Alipotafutwa Minziro kuzungumzia hali hiyo, hakupatikana kutokana na kuwa bize na maandalizi ya mwisho ya mchezo wao wa Kombe la FA dhidi ya Kiluvya United uliochezwa jana Jumanne kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Mbali na changamoto ya mbinu za kiufundi, wapo wachezaji wanaodaiwa kuwa na matatizo ya kiuchezaji huku baadhi yao wakionekana kupoteza morali kutokana na mwenendo wa timu. Hali hiyo imechangia matokeo duni.
Hata hivyo, bado kuna matumaini kwa Minziro endapo ataonyesha mabadiliko katika mechi chache zijazo.
Pamba Jiji inakabiliwa na michezo migumu, ikiwa ni pamoja na dhidi ya Namungo na Fountain Gate, ambazo nazo zinapambana kuepuka kushuka daraja.
Mchuano wa kuwania kubaki Ligi Kuu umekuwa mkali na endapo Pamba Jiji haitajipanga vizuri, inaweza kujikuta ikirejea Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao baada ya kupambana kwa takribani miaka 23 kurejea Ligi Kuu Bara msimu huu.
Je, Minziro ataweza kuokoa nafasi yake na kuibeba Pamba Jiji kutoka kwenye hali mbaya? Hilo litasubiriwa kuona katika michezo ijayo.