Milolongo utumishi wa umma inavyoathiri ndoa, malezi

Dodoma/Dar. Serikali imewataka wakuu wa taasisi na mamlaka za umma kutumia hekima na busara kushughulikia haraka uhamisho wa watumishi wao ili kuepusha athari za kijamii, ikiwemo kuvunjika kwa ndoa na kuharibikiwa kwa watoto.

Sambamba na hilo, imebainisha kuwepo kwa watu wanaojipenyeza kuomba ajira za ualimu ilhali hawana taaluma hiyo, ikidokeza uwezekano wa kuwepo walimu wasio na taaluma husika.

Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, Jumatatu ijayo wizara yake, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, na Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) zitakutana na Umoja wa Walimu Wasiokuwa na Ajira Tanzania kuanzia mwaka 2015 hadi 2023 (Neto) kusikiliza kilio chao.

Simbachawene amesema hayo leo, Jumatatu, Machi 3, 2025, alipohutubia ufunguzi wa kikao kazi na wakuu wa taasisi za umma, kinachofanyika jijini Dodoma.

Katika hotuba yake, amesema wapo watumishi wa umma wenye miaka zaidi ya 20 ya ndoa, lakini hawakuwahi kupata nafasi ya kuishi zaidi ya mwezi mmoja wa likizo na wenza wao.

Hayo yanatokea kwa sababu, kila wanapojaribu kuomba kuhamishiwa walipo wenza wao, wakuu wa taasisi za umma hawashughulikii.

Amejenga hoja hiyo kwa kurejea taarifa aliyopewa ikionyesha kuwa kuanzia Septemba mosi, 2023, ulipoanza kutumika mfumo wa uhamisho wa watumishi wa umma hadi Februari 20, 2025, jumla ya watumishi 21,404 wameomba uhamisho.

Hata hivyo, ni maombi 2,334 pekee ndiyo yaliyofanyiwa kazi, huku taarifa za mfumo zikibaini kuwa maombi 12,069 bado yapo kwa waajiri wa watumishi kwa ajili ya kutolewa uamuzi.

“Jibu lenu ninyi huwa ni rahisi tu, tumepeleka sijui utumishi. Wale watu wakipata nafasi wanakuja kujaa pale ofisini kwangu wakiulizia barua yake ya uhamisho imekwama utumishi. Nani kakwambia ofisa utumishi? Lakini ofisa utumishi barua ameiweka ofisini kwake, hataki kuipeleka,” amesema.

Amesema kufanya hivyo kunapoteza muda wa watumishi wakifuatilia mambo yasiyokuwepo, huku akiwataka viongozi hao wasimamie maombi hayo kwa wakati na kuhakikisha wasimamizi wa kazi wanatekeleza majukumu yao kwa wakati.

“Ni vema ukamwambia, ‘Wewe huwezi kuhama kwa sababu moja, mbili, tatu, hata hivyo, tupe muda tukimaliza kazi hii, tutatafuta mtu mbadala baadaye tutakuruhusu,’” amesema.

Amesisitiza kuwa familia nyingi zinakufa kwa sababu ya wenza kukaa mbalimbali. “Wako watumishi ambao tangu wameanza kazi ndoa ina miaka 20, hajawahi kukaa na mumewe kwa zaidi ya wiki mbili, ukichukua ile ya likizo kwa zaidi ya mwezi mmoja.”

Ameeleza kuwa, “Wewe ofisa utumishi, mkurugenzi, na hasa wa halmashauri, unamzuia huyu kumtekelezea ombi lake la uhamisho. Unajua kabisa amekaa miaka 20 pale. Basi, anapokaribia hata kustaafu, busara ya kawaida ikwambie huyu mtu anahitaji kwenda akaijenge familia yake. Hiyo ni huruma tu.”

Amesema analizungumza hilo kwa sababu, mbali na uongozi, yeye ni baba na babu na anaona hasara ya wenza wanapoishi tofauti na hata watoto wanapoishi mbali na wazazi.

“Mimi nitabaki na hoja yangu hii kwa kuwa sina namna ya kufanya. Siwezi kutumia nguvu, siwezi kuwaamrisha. Mimi narudia kuwaomba, tumieni busara katika eneo hili,” amesema.

Amesema kuna hasara nyingi za kijamii zinazosababishwa na watumishi kukataliwa uhamisho, ingawa viongozi wa utumishi wa umma hawaelewi.

“Kama tukipima kwa thamani ya namna ambavyo jamii inaharibika kupitia eneo hilo tu, nawaambia, makaka na dada zangu, hasara ni kubwa kwa Taifa,” amesema.

Ameiambatanisha hoja hiyo na kile alichoeleza kuwa katika baadhi ya taasisi kumekuwa na tatizo la kujua hata nani anapaswa kufanya nini, wakati wote kunakuwa na muingiliano.

“Wakati mwingine Katibu Tawala wa Halmashauri (DAS) unakuta anamfokea mkurugenzi. Mkurugenzi ni mtu mkubwa sana katika halmashauri. Mkurugenzi wa halmashauri ni sawa na mkurugenzi wa wizarani tu, na pengine mkuu wa wilaya inaweza kuwa sawa,” amesema.

Amesema kumejitokeza mienendo isiyo ya kawaida katika utumishi wa umma, akitaja baadhi ya waajiri kuchagua aina ya watumishi wa kufanya nao kazi.

“Hali hii inasababisha viongozi hata kuwakataa watumishi wanaohamishiwa kwenye maeneo yenu. Huna nafasi ya kumkataa, unampokea. Kama ana changamoto, unazishughulikia, na kama hazingatii, unamchukulia hatua za kinidhamu kwa sababu sheria zipo.”

“Lakini kuna kauli ya jumla kwamba huyu hafai; wewe, kwani unafaa? Wewe aliyekwambia unafaa ni nani? Si umepata bahati tu? Tena si ajabu umepata hicho cheo kwa ujanja ujanja tu,” ameeleza.

Bahati wanazopata viongozi wa utumishi wa umma, amesema, zisiwafanye wajione na haki ya kuwatuhumu wengine kwenye jambo la umma na kujifanya mwema.

“Wengi wanaofanya mambo hayo, tukiwachunguza, ndio mara nyingi ni wala rushwa, wapigaji hao. Watumiaji wabaya wa madaraka kwenye taasisi zao. Kwa hiyo ndugu zangu, hii nchi ni yetu sote. Uwe makini unapojihusisha na masuala ya umma,” amesema.

Amewataka viongozi wa taasisi za umma kuwatumia wenye uwezo na kuwaingiza kwenye mfumo bila kuchelewesha masuala yao ya kiutumishi, ikiwemo kupewa nafasi kama ana sifa.

“Mbaya zaidi ni kung’ang’ana na mtu asiye na sifa. Wewe unang’ang’ana naye tu. Kitakachotokea ukihamishwa wewe kuwa mtendaji mkuu mahala fulani kwa sababu uliwaingiza watu wa kijijini kwenu au uliomaliza nao chuo. Atakapokuja mwingine, naye atafanya hivyo hivyo. Wale uliokuja nao ujue safari imeanza. Jamani, nasema uongo?” amesema.

Kuhusu wanaokaimishwa nafasi za uongozi kwa muda mrefu, amesema wengi wanakumbwa na hilo kwa sababu hawakuwa na sifa za kukaimu nafasi hizo.

“Tunakaimisha watu wasiokuwa na sifa na kuisababishia serikali madeni, lakini madeni hayo hayawezi kulipika kwa sababu anayekaimishwa anapaswa kuwa na sifa hadi apate kibali cha Katibu Mkuu,” amesema.

Mashaka ya walimu feki

Simbachawene amesimulia kilichobainika katika usaili wa walimu, akisema yupo mmoja asiye na taaluma hiyo aliyepenya hadi akaingia kusailiwa.

“Kwenye usaili watu wengine ni wachawi sijui wanapenyaje, yaani mnachuja mtakavyochuja, unajua kuna majamaa yanaingia kwenye usaili wa walimu wakati sio mwalimu, hajawahi kusomea ualimu kabisa.

“Umeweka mtihani anafaulu sasa ukishakuja kwenye usaili wa mdomo ndio anaulizwa hivi ukiwa na darasa unafanyaje yule jamaa anapata nne, wakati huku kwenye kuandika amepata 99,” amesema.

Amesema upo uwezekano wa kuwepo walimu wasio na taaluma kutokana na uzoefu wa kilichojitokeza.

Wanaoghushi barua za uhamisho

Simbachawene amegusia mtandao wa watumishi wa umma waliokuwa wanatumia barua za kughushi kujihamisha kutoka taasisi moja kwenda nyingine.

Katika watumishi hao waliojihamisha kwa kughushi barua, amesema yumo kijana anayemfahamu, lakini hakusita kumfukuza kazi.

“Mmoja kati ya wale aliyejihamisha kutoka Zimamoto akajipeleka TPDC (Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania) ni kijana ninayemfahamu, ni kijana wangu. Kazi nzuri nimemfukuza kazi.

“Nilikuwa naingojea, ngojea tu nilidhani imekufa nini, lakini juzi ananipigia simu, baba, nimefukuzwa kazi, sitarudia tena… Nikamwambia, muombe Mungu akujaalie, tu endelea huko huko,” amesema.

Kujibu malalamiko

Ingawa bado kuna malalamiko ya kuchelewa kwa hatua, amesema viongozi wa utumishi wa umma, hata wakilalamikiwa, hawatoi mrejesho wala hawasikiki wakisema kwa yanayolalamikiwa hadharani.

“Taasisi yako kila siku inasema jambo fulani, lakini wewe hutokei kujibu hata mara moja, huo ni upungufu katika misingi ya utawala bora. Kwa mujibu wa Katiba, misingi ya utawala unatokana na watu,” amesema.

Amesema ukiona jamii inapiga kelele kuhusu eneo au jambo fulani, ni dhahiri kuna tatizo.

“Wanaweza wakakosa lugha nzuri ya kulisema tu, lakini ujue kuna tatizo. Mnapokaa kimya kutokuleta mrejesho kupitia ama mifumo, au kutoka hadharani, hii mnaukosea muhimili muhimu sana katika misingi ya utawala bora,” amesema.

Amewataka viongozi hao, inapotokea hali kama hiyo, wajitokeze kujibu, kueleza, kuelimisha, na wafafanue ili wote waende sawa.

Awali, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Juma Mkomi, amesema malalamiko mengi anayopokea ofisini kwake yanawahusu watumishi wenye changamoto zinazopaswa kutatuliwa na waajiri wao.

Kukutana na Neto

Simbachawene amesema kutokana na baadhi ya taasisi za umma kukataa kutoa ajira za mkataba, imesababisha vijana kununung’unika, na ndiyo maana wameibuka Neto.

“Hawa lazima wasikilizwe, na mimi nilisema waje niwasikilize. Nashukuru wamekubali tena wamejiratibu na nimemwambia Katibu Mkuu nikutane nao Jumatatu ijayo, tuzungumze, tushauriane, tunaweza tukapata jawabu.

“Kwa sababu wao ni wasomi, wameijua hali halisi ya nchi yao, watakuwa na mawazo mazuri, na mimi nawaambieni jambo hili litaisha kwa vijana wale kutupa maarifa sisi Serikali ili tuone tunafanya nini kwa ajili yao,” amesema.

Simbachawene pia, amesema kumekuwepo changamoto ya kutosimamia ipasavyo matumizi ya mifumo iliyosanifiwa kwa ajili ya usimamizi wa rasilimali watu na uwajibikaji.

“Nisisitize zaidi matumizi ya mifumo ya Tehama katika utoaji huduma kwa wananchi wetu, ndiko tulikofika sasa hivi, kwa sababu hiyo inaondoa vishawishi na ulaghai kwa wasiokuwa waaminifu,” amesema.

Changamoto nyingine, amesema, baadhi ya viongozi kutoipa umuhimu rasilimali watu, na mara nyingi wanatumia nguvu kusimamia fedha badala ya watu.

“Kwenye fedha, hata kama zinapotea, lakini unaona nguvu ya kusimamia rasilimali fedha. Lakini kwenye rasilimali watu, ni kama jukumu lililotupwa, na pengine hata ushauri wa ofisa rasilimali watu sio muhimu sana, na wakati mwingine hata ofisi yake haina vitendea kazi, haina vya kutosha.

“Unaweza kumkuta rasilimali watu kati ya wanaopaswa kuwa na usafiri, yeye usafiri wake ni wa ovyo ovyo tu, lakini ndiye anayeangalia rasilimali watu iliyopo katika eneo lako ili ufanye tija ya malengo uliyowekewa katika taasisi yako, huu ni upungufu mkubwa,” amesema.

Amesema sio sawa kutumia rasilimali nyingine bila kuijenga rasilimali watu vema.

“Ndio maana unakuta wananchi wetu wakienda kupata huduma, wanakutana na watumishi waliochoka, ambao wamekata tamaa, kwa sababu hata wakienda kwa ofisa utumishi wao kumwambia jambo, hawezi kulishughulikia vizuri, na yeye anawakoromea tu kwa sababu na yeye ana msongo.

“Msongo ameupata kwa sababu ya taasisi haitambui nafasi na umuhimu wake ipasavyo,” amesema.

Amesema baadhi ya viongozi wa utumishi wa umma hawalitekelezi vema jukumu hilo.