
Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limetoa kibali kwa mwanamitindo wa kimataifa na mrembo wa Tanzania, Millen Magese kuandaa mashindano ya Miss Universe Tanzania.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Basata, Dk Kedmon Mapana amesema baraza hilo kama walezi na wasimamizi wa karibu wa tasnia ya urembo, ulimbwende na utanashati wameamua kumpa baraka zote Millen Magese kuandaa mashindano hayo nchini.
Amesema ataandaa mashindano hayo kupitia Kampuni yake ya ya Millen Privé & Co. Lifestyle Bespoke Luxury Lifestyle & Hospitality Management.
“Tunajivunia na wale wanaofuatilia Millen Magese yuko nje ya nchi anakaa Marekani lakini bado moyo wake unasema kwa nini asirudi nyumbani afanye jambo kwa maendeleo ya nchi yetu ya Tanzania, lakini pia kwa maendeleo na ustawi wa Basata.”
“Hivyo tunamtakia kila la heri na tunategemea mambo yetu yatakuwa mazuri kwamba kazi hii Millen unaiweza lakini na sisi kama Tanzania tutafurahi kuona mashindano ya ulimbwende Miss Universe tuna mwakilishi kutoka Tanzania,”amesema Dk Mapana.
Aidha amesema mashindano ya Miss Universe yana mambo mengi na ndio maana mbali ya kumpatia baraka na kibali cha kuyaandaa wamemkabidhi mwongozo wa maadili katika kazi za sanaa, na kumsisitizia wanapofanya mashindano ya ulimbwende wasisahau kuna mila na desturi zetu.
“Tuhakikishe kwamba kama Tanzania tunapokwenda huko nje tunasema huyu mrembo anatoka Tanzania na anapambanua vipi hasa suala la maadili, hivyo tunatarajia mwongozo huu tuliomkabidhi Millen atautumia vizuri na sisi Basata tutahakikisha jambo hili linakwenda kutekelezeka vizuri.”
Kwa upande wake Millen ameishukuru Basata kumpatia baraka na kibali cha kuandaa na kuratibu mashindano ya Miss Universe Tanzania kupitia kampuni yake.
“Nashukuru kwa kupata kibali cha Miss Universe Tanzania kutoka Miss Universe Organization na kwa sasa pia nimepata kibali cha hapa Tanzania kupitia Basata, hivyo nina baraka zote mbili. Kwa kushirikiana na Basata na wadau wote nchini tunategemea safari hii itakuwa ni suala nzima la kunyanyua hii sanaa nzima ya mambo ya ulimbwende Tanzania.”
“Kwetu hii ni nafasi muhimu tutatumia platform hii ya Miss Universe kuitangaza nchi yetu kwani watu zaidi ya bilioni moja kwa wakati mmoja hufuatilia na nchi zaidi ya 174 zimekuwa zikishiriki mashindano haya,”amesema Millen.
Amesisitiza ulimbwende bado una nafasi kubwa sana na ndio jukwaa ambalo linaweza kukutangaza kwa ukubwa nje ya nchi, huku akitumia nafasi hiyo kumpongeza Miss Universe Tanzania mwaka 2024 Judith Ngussa na kuahidi kushirikiana naye katika mashindano hayo kwani ana uzoefu maana alishafika Miss Universe World.
“Tunamkaribisha Miss Universe mwaka 2024 Judith Ngussa kuungana nasi na kufanya kazi anafahamu zaidi mashindano haya na wasichana wengi wanamuangalia na wanapenda kumuona katika safari hii nzima ya kumtafuta mlimbwende wa mwaka huu, ikiwezekana Judith asaidie kumuongoza,”amesema Millen.
Awali Miss Universe 2024, Judith Ngussa amesema amefurahi Millen kupewa leseni ya kuandaa mashindano hayo na kusisitiza yuko tayari kumuunga mkono katika kufanikisha mashindano hayo.