Pambizoni mwa mkutano wa wakuu wa nchi za BRICS huko katika mji wa Kazan nchini Russia, Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi shiriki ambapo amesisitiza haja ya kuzingatiwa mitazamo ya pande kadhaa katika mfumo wa kimataifa.
Mkutano wa 16 wa kilele wa kundi la BRICS ulifanyika kuanzia Jumanne hadi Alhamisi huko katika mji wa Kazan, nchini Russia ambapo Rais Masoud Pezeshkian alishiriki katika mkutano huo kama mmoja wa viongozi wa nchi wanachama wa BRICS na kwa mwaliko rasmi wa Rais Vladimir Putin wa Russia.
Mbali na kuhutubia vikao mbalimbali vya mkutano huo, Rais Pezeshkian amekutana na kushauriana na marais wa nchi mbalimbali kuhusu masuala tofauti. Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye aliandamana na Rais Pezeshkian katika safari hiyo nchini Russia amesema kuhusu mikutano ya pande mbili ya Rais Pezeshkian pambizoni mwa kikao hicho kwamba: “Mikutano ya pande mbili ilifanyika pambizoni mwa kikao hicho, lakini duru hii ilikuwa na kipengele maalum ambacho ni umuhimu wa mikutano ya pande mbili. Pezeshkian alifanya mikutano ya pande mbili na Marais wa Russia, Belarus, Venezuela, China, Misri, Afrika Kusini, Bolivia, Mawaziri Wakuu wa India na Armenia, na vile vile Waziri Mkuu wa UAE.”

Moja ya mihimili mikuu ya vikao vya pande mbili vya Rais Pezeshkian na viongozi wa nchi tofauti ni mgogoro wa hivi sasa katika eneo la Asia Magharibi na jinai za utawala katili wa Israel unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu, dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza na Lebanon. Sayyid Abbas Araghchi aidha amesema, ulazima wa kupunguzwa mivutano katika eneo, kusitishwa jinai za utawala wa Kizayuni na ulazima wa kusitishwa mapigano na kushughulikia hali ya wakimbizi ni baadhi ya mambo yaliyojadiliwa na kupewa uzito maalumu katika vikao hivyo.
Mikutano ya pande mbili ya Rais Pezeshkian kando ya mkutano wa kilele wa BRICS ni yenye umuhimu kadhaa. Umuhimu wa kwanza ni kwamba, Rais Pezeshkian alikutana na kushauriana na wakuu wa nchi katika mabara manne ya Asia, Ulaya, Afrika na Amerika. Kila moja ya serikali hizi ni kati ya nchi muhimu katika kanda na zingine katika kiwango cha kimataifa. Huku mikutano hii ikithibitisha uongo wa madai kuwa Iran imetengwa katika ngazi ya kimataifa, lakini pia inachukuliwa kuwa ni fursa ya kuongeza maingiliano ya pande mbili hususan katika uga wa kiuchumi. Kuhusiana na hilo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, masuala yote ya pande mbili yalipitiwa upya katika vikao hivyo na kwamba Iran ina miradi muhimu ya pande mbili na kila moja ya nchi hizo. Kupanuliwa mahusiano, biashara na matumizi ya mbinu mpya katika biashara na kuondolewa vikwazo vya kidhalimu vilivyowekwa na Marekani, yote hayo yalijadiliwa katika mikutano hiyo.
Suala jingine muhimu ni kwamba, Rais Pezeshkian na viongozi wa baadhi ya nchi katika kikao cha Kazan walisisitiza kwa uwazi ulazima wa kuelekea kwenye mfumo wa pande kadhaa katika ngazi za kimataifa na kukabiliana na mfumo wa upande mmoja wa Marekani. Kwa hakika maslahi ya nchi nyingi wanachama wa BRICS ni kukabiliana na siasa za upande mmoja za Marekani katika ngazi za kimataifa kwa sababu nchi hiyo inatumia vibaya siasa hizo kuzishinikiza nchi huru katika nyanja mbalimbali hususan za kiuchumi. Kuhusiana na suala hilo, Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: “Hivi sasa BRICS inabadilika kuwa kambi mpya yenye nguvu katika uga wa kimataifa. Kambi hii inajumuisha nchi ambazo zinapinga siasa za upande mmoja na zinataka kubuni mfumo wa haki ulimwenguni ambao unazingatia mitazamo ya pande nyingi isiyohodhiwa na kudhibitiwa na taasisi za Magharibi.”