Mikopo ya kidijitali yafikia Sh4.22 trilioni, mahitaji yakiongezeka

Dar es Salaam. Miamala ya mikopo ya kidijitali nchini Tanzania imeshuhudia ongezeko kubwa mwaka 2024, ikiongezeka kwa asilimia 91.49 hadi kufikia Sh4.22 trilioni kutoka Sh2.20 trilioni mwaka 2023.

Idadi ya miamala pia iliongezeka kwa asilimia 64.77, ikipanda kutoka milioni 163.42 hadi milioni 269.30, kwa mujibu wa Ripoti ya Mwaka ya Mfumo wa Malipo wa Taifa iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), 2024.

Ongezeko hilo kubwa linaonyesha kukua kwa mahitaji ya mikopo kwa njia ya simu ambayo imekuwa ni nyenzo muhimu ya kifedha kwa Watanzania wengi.

Majukwaa kama Kamilisha, Timiza, M-Pawa, Agent Overdraft, Bustisha, Nivushe, Digital Salary Advance, Boom Advance, Songesha na Kibubu yamekuwa na mchango mkubwa kwenye kutoa mikopo ya haraka kwa masharti nafuu.

Akizungumza na gazeti dada la The Citizen, Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Mwinuka Lutengano, anahusisha ongezeko la mikopo ya kidijitali na urahisi wake wa kupatikana.

“Huduma za kifedha za simu zimeziba pengo kwa watu wengi ambao awali hawakuwa na huduma za benki. Uwezo wa kupata mkopo bila kwenda benki umefanya mikopo ya kidijitali kuwa chaguo bora kwa watu binafsi na wafanyabiashara wadogo,” amesema.

Ameongeza kuwa mikopo ya kidijitali imechangia ujumuishaji wa kifedha, hasa vijijini ambako huduma za kibenki ni chache.

“Watanzania wengi sasa wanategemea mikopo ya simu kwa dharura, uwekezaji wa kibiashara, na mahitaji ya kila siku. Licha ya faida hizi, ni muhimu kuhakikisha kuwa wakopaji wanaelewa hatari zinazohusika na kuepuka kuingia katika janga la madeni,” amesema.

Ongezeko la mikopo ya kidijitali linadhihirika katika sekta mbalimbali, huku wafanyabiashara wadogo na watu binafsi wakitegemea mikopo ya simu kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umaskini (Repoa), Dk Donald Mmari, ameeleza kuwa mikopo ya simu imekuwa chachu ya shughuli za kiuchumi.

“Urahisi wa kupata mikopo umewezesha biashara kukua, kuchangia ajira na uthabiti wa kiuchumi. Wajasiriamali wengi, hususan wa sekta isiyo rasmi sasa wana akiba ya fedha inayowasaidia kudhibiti hatari na kuwekeza kwenye biashara zao,” amebainisha.

Hata hivyo, anatahadharisha kuwa bila udhibiti sahihi, baadhi ya wakopaji wanaweza kupata ugumu wa kulipa madeni yao.

“Watu wengi wanachukua mikopo mingi bila kufikiria athari za muda mrefu kwa uthabiti wao wa kifedha. Ni muhimu kuimarisha hatua za kulinda watumiaji na kuhakikisha kuwa mikopo ya kidijitali inatumika kwa uwajibikaji,” amesema.

Dk Mmari ameeleza kuwa licha ya manufaa ya mikopo ya kidijitali, uendelevu wake unategemea elimu ya kifedha na usimamizi wa kisheria.

“Tunahitaji sera zinazowalinda wakopaji dhidi ya ukopeshaji wa kinyonyaji na kuhakikisha kuwa viwango vya riba vinabaki kuwa vya haki. Programu za elimu ya kifedha zinapaswa kuanzishwa kusaidia watu kusimamia mikopo yao kwa ufanisi,” amesema.

Ingawa mikopo ya kidijitali imeleta nafuu ya kifedha kwa Watanzania wengi, wasiwasi juu ya ongezeko la madeni unaendelea kukua. Baadhi ya wakopaji wanajikuta wakichukua mikopo mipya kulipa mikopo ya zamani.

Akizungumzia hili, mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Daudi Ndaki amesema  kuwa kasi na urahisi wa kukopa vinaweza kusababisha matatizo ya kifedha ikiwa hayatadhibitiwa ipasavyo.

“Tofauti na mikopo ya benki ya kawaida, mikopo ya simu mara nyingi hupatikana ndani ya dakika chache. Urahisi huu, ingawa ni mzuri, pia huongeza hatari ya kukopa kiholela. Watu wengi hawaelewi kikamilifu masharti ya marejesho, jambo linalosababisha ugumu wa kulipa mikopo yao,” ametahadharisha.

Wakati mikopo ya kidijitali ikishuhudia ongezeko kubwa, miamala ya akiba ya kidijitali imeonyesha mwenendo wa mchanganyiko.

Ripoti inaonyesha kuwa idadi ya miamala ya akiba ya kidijitali ilipungua kwa asilimia 1.72, ikishuka kutoka milioni 47.28 mwaka 2023 hadi milioni 46.47 mwaka 2024.

Hata hivyo, thamani ya jumla ya miamala ya akiba ya kidijitali iliongezeka kwa asilimia 10.16 hadi Sh1.21 trilioni.

Dk Isack Safari kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine Tanzania (SAUT) ameeleza kuwa ingawa watu wachache wanafanya miamala ya akiba ya kidijitali, ongezeko la thamani linaashiria mabadiliko katika tabia ya kuweka akiba miongoni mwa Watanzania.

“Watu wanaweka kiasi kikubwa zaidi kwa kila muamala, jambo linaloonyesha kuongezeka kwa imani katika majukwaa ya akiba ya kidijitali. Watanzania wengi wanaanza kuona thamani ya kuweka akiba kwa utaratibu badala ya kuhifadhi pesa taslimu,” amesema.

Hata hivyo, Dk Safari amesisitiza kuwa jitihada zaidi zinahitajika ili kuhamasisha utamaduni wa kuweka akiba.

“Ingawa majukwaa ya akiba ya kidijitali yanazidi kupata umaarufu, watu wengi bado wanapendelea kukopa badala ya kuweka akiba. Taasisi za kifedha zinapaswa kuanzisha vivutio zaidi vya kuweka akiba, kama vile programu za zawadi kwa waweka akiba wa mara kwa mara,” anasema.

Mhadhiri wa masoko katika Taasisi ya Uhasibu Tanzania, Dorence Kalemile amehusisha ongezeko la mikopo ya kidijitali na mikakati ya masoko ya wakopeshaji wa simu, akisisitiza urahisi wa upatikanaji na masharti machache.

“Wakopeshaji wa simu wamejipanga kama suluhisho la haraka la kifedha, hasa kwa wafanyabiashara wadogo na dharura,” amesema.

Hata hivyo, ameonya kuwa matangazo makubwa yanaweza kuchochea ukopaji usio na nidhamu.

Mtaalamu wa masoko ya kidijitali, Justus Mwita, amehusisha ukuaji wa mikopo ya kidijitali na matumizi ya masoko yanayotegemea data na ofa za mikopo zinazolengwa kwa wateja binafsi.

“Wakopeshaji wanachambua tabia za matumizi ili kubinafsisha mikopo, jambo linaloongeza imani na matumizi,” ameeleza, akionya kuwa “matangazo ya mikopo kupita kiasi bila elimu ya kifedha yanaweza kusababisha mizunguko ya madeni.”

Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa thamani ya malipo ya huduma kupitia simu za mkononi imefikia Sh198.85 trilioni katika mwaka 2024 kutoka Sh154.7 trilioni katika mwaka uliotangulia huku idadi ya mawakala ilifikia 1,475,281 mwaka 2024 kutoka 1,240,052, mtawaliwa.

Uchambuzi unaonyesha kuwa, mwaka 2024, miamala ya mtu kwa mtu iliongezeka hadi kufikia milioni 479.11 yenye thamani ya Sh15.702 trilioni ikilinganishwa na miamala milioni 364.36 yenye thamani ya Sh11.323 trilioni iliyokuwapo mwaka uliotangulia.

Malipo kwa Biashara (P2B) pia ukuaji wake ulishuhudiwa kuanzia mwaka 2020, ambapo idadi ya miamala iliongezeka kwa asilimia 28.52 na thamani ya miamala ilikua kwa asilimia 45.76 mwaka 2024.

Jumla ya miamala ya malipo ya huduma na bidhaa bilioni 1.74 yenye thamani ya Sh26.602 trilioni ilishuhudiwa mwaka 2024.

Ongezeko hili kwa mujibu wa BoT linaonyesha kuongezeka kwa matumizi ya malipo ya kidijitali kwa wafanyabiashara na kuashiria mabadiliko makubwa kuelekea miamala ya biashara yenye ufanisi zaidi na inayopatikana kwa urahisi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *