Dar es Salaam. Katika hali isiyo ya kawaida mikoko iliyopo Kijichi, eneo ambalo Mto Mzinga unaingia Bahari ya Hindi, wilayani Temeke imekauka.
Ingawa ukubwa wa eneo lililoathiriwa haujatambulika, uchunguzi umebaini maeneo mengi pembezoni mwa mto huo yenye uoto wa mikoko yameathirika.
Si mikoko pekee iliyokauka, katika baadhi ya maeneo huwezi kuona uoto, viumbe wa majini kama vile kaa, vyura na ndege, hivyo kuashiria athari za kimazingira.
Mikoko ambayo huota kwenye makutano ya maji-chumvi na maji-baridi, husaidia kulinda mazalia ya viumbe wa majini, kuzuia mmomonyoko wa fukwe ya bahari na kupunguza ukubwa wa mawimbi, kama inavyoelezwa na mtaalamu wa mazingira, Julius Moshi.
Kwa mujibu wa Moshi ambaye ni ofisa kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kukauka kwa miti hiyo kunaathiri mazalia ya samaki na viumbe wengine, kuchochea mmomonyoko wa fukwe, mafuriko na kuruhusu mawimbi ya bahari yapige kwa ukubwa unaoweza kuhatarisha maisha ya wananchi.
Ukiachana na faida hizo, Utafiti wa Chuo Kikuu cha Umoja wa Mataifa (UNU) na Taasisi ya Mazingira na Usalama wa Binadamu wa mwaka 2020, unaonyesha misitu ya mikoko ina ufanisi zaidi katika kuondoa hewa ukaa, hivyo kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa sababu ya umuhimu wa misitu hiyo, Serikali inaandaa mkakati wa kitaifa wa usimamizi wa mikoko unaotarajiwa kuzinduliwa Julai, 2025.
Nini kimetokea
Wakati wananchi eneo la Kijichi waliozungumza na Mwananchi wanasema kumwagika kwa mafuta baada ya kupasuka Bomba la Mafuta la Tanzania na Zambia (Tazama) mwaka 2024 ni sababu ya mikoko kukauka, Tazama wanakana hilo.
Kwa upande wake, Tazama inakiri mafuta kumwagika, lakini inasema haihusiki na kukauka kwa mikoko kwani yaliyomwagika yalishaondolewa. Pia inaeleza hakuna tafiti inayoonyesha kama kukauka kwa miti hiyo chanzo chake ni mafuta.
Ikiwa ni takribani mwaka mmoja tangu kuibuka taharuki eneo la Kijichi, mkoani Dar es Salaam, Shakira Mohamed, mjumbe katika eneo la Dampo, lililopo Benki Club- Bukorani anasema:
“Mafuta yalifika huku (akionyesha eneo ambalo mikoko imekauka makadirio ya mita 50 kutoka kwenye mto)”
Shakira anasema katika kipindi hicho, vijana wenye madumu walikwenda kuchota mafuta.

“Walikuwa wanachota na sponji, wanakamua. Wakija huku (nchi kavu) unawamwagia maji masafi na wanaoga kwa kuwa walikuwa wakiwashwa,” anasema.
Shakira anasema anaamini baada ya mafuta kumwagika ndipo mikoko imekauka.
“Walikufa samaki, ndege hata hawa kaa unaowaona sasa hawakuwepo,” amesema.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Ezeda Mwamnyani, bomba lilipasuka Mbagala Kingugi (takribani kilomita tatu mpaka baharini) Aprili, 2024 na kuanza kumwaga mafuta kwenye Mto Mzinga.
Kwa mujibu wa Tazama, bomba lilipasuka Mbagala ila hawakueleza eneo husika.
“Mikoko ilianza kukauka miezi kadhaa baada ya mafuta kumwagika, yalikuwa mengi kiasi kwamba watu walikuwa wanachota na kujaza madumu,” amesema Mwamnyani.
Ezeda anasema wananchi hawakuathirika zaidi ya harufu mbaya ya mafuta iliyokuwepo wakati huo. Anasema ilichukua takribani siku nne hadi mafuta kupunguza.
Mkulima pembezoni mwa mkondo wa Mto Mzinga, Adam Myamba anasema kabla ya mafuta kusambaa ilikuwa nadra kuona mkoko ukikauka.
“Unaweza kuuona mmoja umekauka hadi uone mwingine itakuchukua muda. Lakini hata sisi hatuna uhakika kwamba mafuta ndiyo yameikausha au vinginevyo.
“Tunasema mafuta kwa sababu ilianza kukauka muda mchache baada ya mafuta kusambaa, kwa nini haikukauka kabla,” anasema.
Anasema wakati mafuta yakiwa yamesambaa hata wananchi waliotumia maji ya Mto Mzinga walipata tabu.
“Mafuta yalikuwa mengi na yenyewe yanakaa juu maji chini, usingeweza kutumia maji maana yalikuwa na mafuta mengi,” amesema.
Mjumbe wa Mtaa wa Benki Club- Bukorani, Amina Salum amesema mafuta yalianza kusambaa Aprili, 2024.
Amesema viongozi wa serikali ya mtaa walijitokeza na kuwaonya wananchi wasiende kuyachota.
“Walionywa kwa sababu ni hatari kwa usalama wao, lakini bado watu walikwenda kuchukua mafuta,” amesema.
Anasema hapakuwa na madhara yaliyoshuhudiwa kwa binadamu zaidi ya kukauka kwa mikoko kulikoanza mwezi mmoja baada ya mafuta kwisha.
Anasema hakuwahi kuona mafuta yakiondolewa zaidi ya wananchi kuchota na madumu yakapungua na baadaye kwisha.
Tazama yajitenga
Akizungumzia hilo, Ofisa Afya na Mazingira wa Tazama, Hija Masoud amesema sheria inawataka linapopasuka bomba wafanye usafi kuhakikisha mafuta yote yanaondolewa.
Kwa mujibu wa Masoud, usafi wanalazimika kuufanya chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na ndivyo ilifanyika.

“Sisi tunatakiwa kufanya usafi na tumefanya kuhakikisha mafuta yote yaliyomwagika yanaondolewa. Sijajua hasa kama kukauka kwa mikoko hiyo kuna uhusiano na mafuta hayo au vinginevyo,” amesema.
Amesema kuna sababu zaidi ya mafuta kwa mikoko kukauka na kwamba, hajajua kama hali hiyo imechochewa na kupasuka kwa bomba hilo mwaka 2024.
Akizungumzia kilichotokea Kijichi, Ofisa Tafiti na Mtaalamu wa Jiolojia ya Bahari wa NEMC, Clarance Nkwera amesema tukio hilo limetokea muda mrefu na baraza limechelewa kupata taarifa.
Hatua ya baraza kuchelewa kupata taarifa, anasema imesababisha muhusika asijulikane haraka.
“Navyokwambia hivi juzi (Machi 28, 2025) ndiyo nimepata taarifa ya uharibifu huo, tutakwenda kufanya ukaguzi kuona kiwango cha athari na tutawahoji wananchi wa eneo husika kujua mhusika na tutaona kama ni kwenda mahakamani au vinginevyo,” amesema.
Amesema kwa kawaida wakichelewa kupata taarifa, huwa wanaingia kazini kufanya tathmini ya uharibifu kwa kujionea na kuuliza wananchi kujua kama ni mafuta yametoka kwa nani.
Anasema katika kesi kama ya Kijichi, mara nyingi wanaishia kufanya tathmini ya kina kujua nini sababu, kiwango cha uharibifu, kisha wanaandika ripoti na kupendekeza cha kufanyika kwa uharibifu uliofanyika.
Nkwera anasema kwa taratibu za baraza hilo unapotokea uharibifu wa namna hiyo, atatafutwa aliyehusika na kupigwa penati itakayotokana na kiwango alichoharibu.
Kabla ya adhabu, anasema NEMC inapima kitaalamu kuangalia kiwango cha uharibifu uliofanyika na kutathmini huduma za kiikolijia zilizoharibiwa ni sawa na gharama kiasi gani kwa fedha.
“Gharama itakayopatikana baada ya kupima na kutathmini, ndiyo atakayotozwa mtu au kampuni iliyohusika na uharibifu husika,” anasema.
Namna nyingine, anasema baraza linamsimamia aliyehusika na uharibifu, kuhakikisha anaondoa mafuta yote, kisha atalazimika kurekebisha tatizo alilosababisha, ikiwemo kupanda mikoko na kuisimamia hadi ikue kwa gharama zake.
Mhifadhi Misitu, Temeke na Kigamboni wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Selewin Regie amesema tayari jambo hilo limeshafanyiwa kazi kwa hatua za awali.
Amesema utaratibu wao wa kazi unahusisha kufanya uchunguzi na kuwasilisha taarifa ngazi ya kanda na baadaye Taifa, kazi ambayo imeshafanyika.
“Kwa hiyo kwetu limeshavuka tumelishughulikia kwa kufanya uchunguzi na kuwasilisha taarifa kwa ngazi nyingine na wadau wengine kwa sababu wengi wanahusika. Wadau hao nao wanalishughulikia na likifika mwisho nasi tutajulishwa,” amesema.
Katika hatua ya sasa, anasema hakuna yeyote anayeweza kutoa taarifa kwa kuwa jambo bado linaendelea kushughulikiwa na mamlaka za juu.
Athari zaidi
Mtaalamu wa Mazingira, Julius Moshi anasema mikoko ni kiungo muhimu na msaada katika maeneo ya bahari na vyanzo vingine vya maji.
Anasema hatua ya mikoko kukauka inahatarisha uhai wake kwamba itashindwa kuota mingine katika eneo hilo, hivyo ni muhimu chanzo kiangaliwe kuepuka madhara zaidi.
Anatahadharisha athari hizo zisije kuwapo eneo lingine la mikoko hivyo ikaendelea kukauka.
Si mara ya kwanza
Si mara ya kwanza kwa bomba hilo kupasuka. Mei 17, 2023 mtandao wa Lusakatimes.com uliripoti Zambia kupoteza zaidi ya tani milioni moja za mafuta kutokana na kupasuka kwa bomba la Tazama mkoani Mbeya.
“Kupasuka kwa bomba la mafuta kulipotokea kilomita 839 karibu na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST) huko Iyunga, Mbeya, kulisababisha kumwagika kwa takriban lita milioni moja za dizeli yenye kiwango cha chini cha salfa (LSG)” ilisema ripoti hiyo.
Tukio hilo lilitokea Mei 15, 2023, baada ya mkandarasi aliyekuwa akifanya kazi kwa niaba ya Tarura –(Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini) kuharibu bomba hilo kwa bahati mbaya wakati wa shughuli za ujenzi wa barabara.
Bomba la Tazama linamilikiwa kwa ushirikiano wa Serikali za Zambia (asilimia 67) na Tanzania (asilimia 33).