Mikel Arteta aanza kulia lia

Milan, Italia. Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amekosoa maamuzi ya mwamuzi wa mchezo wao dhidi ya Inter Milan kuwapa penalti wapinzani wao na amesisitiza wao pia walihitajika kupewa penalti.

Arsenal ambayo imepoteza kwa kichapo cha bao 1-0 katika mchezo huo uliopigwa dimba la Giuseppe Meazza imepata vichapo vitatu katika mechi sita za mwisho za michuano yote.

Arteta anaamini penalti ambayo Inter iliipata baada ya Mikel Merino kushika mpira katika eneo la 18, kutokana na shuti la Hakan Calhanoglu haikuwa sahihi na kama ilitolewa kwa wapinzani wao, ilibidi wao pia wapate penalti kutokana na tukio la Merino kupigwa kichwani na kipa wa Yann Sommer.

“Hatukutendewa haki. Sielewi kwa nini iliuamuliwa kuwa ni penalti, hakukuwa na kosa, mikono ilikuwa karibu sana na mwili wake. Hakuwa na namna ya kufanya ili asiuguse mpira, tuliambiwa mwanzoni mwa msimu tukio la aina ile haitakuwa penalti lakini leo ilikuwa hadithi tofauti ingawa kama waliweka ile kuwa ni penalti ile ya Merino kupigwa kichwani pia ilipaswa kuwa ni penalti,” alisema Arteta baada ya mchezo huo na kuongeza kwa sasa wanajiandaa na mchezo wao ujao dhidi ya Chelsea.

Arteta anaamini wachezaji wake walicheza vizuri sana dhidi ya Inter na kama wakifanya hivyo kwa Chelsea basi kuna asilimia nyingi wataibuka na ushindi.

Gwiji wa Arsenal na mchambuzi wa TNT, Martin Keown pia alizungumza kuhusu tukio hilo, haamini ilikuwa ni penalti.

“Unapaswa kuweka mkono wako wapi katika hali kama ile? Nani alitunga sheria hizi? Je, waliotunga waliwahi kucheza mpira?”

Arsenal ambayo itacheza na Chelsea Jumapili ya wikiendi hiil itangia katika mchezo huo ikiwa na hatihati ya kuwakosa baadhi ya wachezaji wake muhimu ikiwemo Kai Havertz aliyeonekana akuvuja damu baada ya kuumia katika mchezo huo.