Mikakati kuimarisha kilimo biashara Zanzibar

Unguja. Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar imesema itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji ili kuimarisha kilimo cha biashara visiwani humo.

Hayo yamesemwa leo Machi 12, 2025 na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Ali Khamis Juma wakati wa utiaji saini wa makubaliano ya uanzishwaji wa mradi wa kuimarisha kilimo biashara nchini na kampuni ya Globespan kutoka Uingereza.

Amesema, lengo la makubaliano hayo ni kuwaleta wataalamu wa kilimo duniani na kuwajengea uwezo wakulima, mabibi na mabwana shamba kisiwani humo ili kupata mbinu bora za kufikia kilimo cha biashara.

“Mradi huo utaweza kujenga vituo vya kuchakata na kutoa maarifa ya shughuli za uzalishaji wa mazao ya kilimo cha biashara, pamoja na wakulima kupata fursa ya kitaalamu kwa ajili ya kununua bidhaa zao,” amesema Juma.

Ameeleza kuwa, makubaliano hayo yataondoa changamoto zinazozorotesha uzalishaji wenye tija na kuongeza wigo wa upatikanaji wa ajira kwa vijana, wanawake na masoko ya uhakika ya mazao ya wakulima.

Pia, Ali amewasisitiza watendaji wa wizara hiyo kuhakikisha wanasimamia vyema miradi itakayoanzishwa ili ilete tija zaidi kama yalivyo malengo ya Serikali.

Vilevile, amesema Serikali imeendelea kuwahakikishia washirika wote wa maendeleo juu ya usalama wa miradi inayoanzishwa Zanzibar kuwa ipo salama kwa manufaa ya pande zote mbili.

Awali, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara kutoka Kampuni ya Globespan, Alistair Johnston amesema mpango wa kukuza biashara ya kilimo na mauzo kwa wakulima wa Zanzibar unaleta uwekezaji mkubwa kwenye mbinu za kisasa za kilimo, kuanzisha mashamba ya kufundishia (hub farms), vituo vya usindikaji mazao na miundombinu ya mauzo ili kuongeza uzalishaji wa mazao.

“Uwekezaji huo unatarajiwa kuleta faida za kiuchumi, na kuiweka Zanzibar kuwa kitovu cha biashara ya mazao ya kilimo na viwanda na kuongeza fursa za mapato kwa wakulima,” amesema Johnston.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *